Breaking News

DC MGANDILWA AFUNGA VIWANDA VYA WACHINA KIGAMBONI, KUFUATIA UKWEPAJI WA KODI ZA SERIKALI

Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe Hashim Mgandilwa, leo tarehe 20/6/2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha plastic cha Ruider Plastic Limited kinachomilikiwa na raia mwenye asili ya China.

DC Mgandilwa aliyeambatana na Mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni Ndg Steven Katemba, walikagua na kugundua mambo mbalimbali yakiwemo ya kiwanda hicho kuendesha shughuli zake pasipo kufuata taratibu za nchi kikamilifu na baadhi ya mianya ya ukwepaji wa kodi.

Baada ya kutembelea eneo la kiwanda ili kujionea shughuli za uzalishaji, Msafara huo ulioongozwa na DC Mgandilwa ulibaini kuwa katika eneo hilo kuna viwanda tofauti Saba vinavyozalisha bidhaa tofauti tofauti.
Viwanda vilivyobainika ni pamoja na kiwanda cha kutengeneza mabomba ya maji ya plastic, kiwanda cha kutengeneza mikeka, kiwanda cha kutengeneza bodi za dari (Ceiling board), kiwanda cha kutengeneza mifuko ya plastic, kiwanda cha kutengeneza maboksi ya plastic kwa ajili ya kutunza vitu vya baridi, kiwanda cha kuyeyusha chupa za plastic, na kiwanda cha kutengeneza mito ya kulalia.

Viwanda vyote hivyo Saba vinafanya shughuli za uzalishaji katika eneo moja na huku kiwanda kinacholipa kodi za serikali kikiwa ni kimoja tu nacho kikisuasua kulipa kama inavyostahili.

Baada ya kutembelea viwanda vyote hivyo, DC Mgandilwa amewataka wamiliki wa viwanda hivyo kusitisha uzalishaji wake mara moja leo hii.

DC Mgandilwa amesema kusimama kwa shughuli za uzalishaji unatoa mwanya kwa timu kutoka mamlaka ya mapato (TRA) na Manispaa ya Kigamboni ambao amewaagiza kuweka kambi katika viwanda hivyo kuanzia kesho ili kupitia nyaraka zote na kubaini kiasi cha mapato ambayo serikali imekuwa ikiyapoteza tangu waanze uzalishaji.

DC Mgandilwa ameagiza kuwa baada ya tathimini hiyo kukamilika pesa yote ambayo serikali imekuwa ikipoteza tangu kuanzishwa kwa viwanda hivyo ilipwe mara moja iwezekanavyo na ndipo uzalishaji uendelee kwa kufuata taratibu zote za serikali.

Inakadiriwa kuwa kiwanda kimoja kilitakiwa kulipa Sh 101 milion kwa mwezi hivyo kuifanya serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Shilingi Milioni 700 kwa mwaka.

No comments