TUNDU LISSU KUKOMALIA VYETI FEKI VYA BASHITE. AUNGANA NA WANASHERIA WENZAKE KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI
Wakili
Tundu Lissu na wenzake wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelikomalia
vilivyo sakata maarufu la Bashite linalohusiana na tuhuma za kughushi vyeti vya
kielimu linalomkabili mmoja wa wakuu wa mikoa kwa kulifikisha kortini ili
lipatiwe ufumbuzi.
Aidha,
Lissu na wenzake hao wamedhamiria kuona kuwa kigogo huyo anayetuhumiwa kuliacha
jina lake halisi la Daudi Albert Bashite kutokana na matokeo mabovu ya
sekondari na kutumia jina la mtu mwingine, achukuliwe hatua za kisheria ikiwamo
kufungwa jela kwa kosa la kughushi ikiwa itathibitika kuwa ana hatia.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu ambaye ni Rais wa TLS,
alisema uamuzi huo wa kulifikisha mahakamani suala la Bashite umetokana na
maazimio ya baraza la uongozi la chama hicho, lengo likiwa ni kulinda utawala
wa sheria na uwajibikaji nchini.
Tofauti
na matarajio ya baadhi ya watu, sakata hilo la Bashite halikupatiwa jibu
kutokana na ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma
iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa kutowagusa viongozi wa kisiasa
wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na madiwani.
Katika
kufanikisha nia hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine wa chama hicho
wakiwamo Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen Kuwayawaya, alisema
miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS kufungua mashtaka binafsi ya
jinai dhidi ya mkuu huyo anayedaiwa kuitwa Bashite.
Aliongeza
kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai likiwamo
hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki haitachukua miezi bali
ni wiki mbili au tatu.
“Kifungu
cha 128(2) cha sheria ya Mwenendo wa jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania
kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, kampuni au mashirika kama TLS)
kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale anapoamini kuna sababu za
msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai limetendwa,”alisema Lissu, akielezea
vifungu wanavyotumia kufikisha suala hilo kortini.
Alisema
dhana ya utawala wa sheria ina maana pana na kwamba, pamoja na mambo mengine,
siyo tu kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia kila mtu bila kujali
cheo au nasaba na hali yake kiuchumi na jamii, yuko chini ya udhibiti wa sheria
za kawaida za nchi na hivyo yuko pia chini ya mamlaka ya mahakama za kawaida.
“Kuna
tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo wa mkoa ametumia vyeti vya shule ya
sekondari visivyokuwa vyake. Yeye… ni Daudi (Albert) Bashite,” alisema Lissu,
akiongeza kuwa jina linalotumiwa sasa na mkuu huyo linadaiwa kuwa mwenyewe yupo
na ndiye mwenye vyeti halisi, na kitendo hicho ni kosa la jinai.
Akifafanua
zaidi, Lissu alisema kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria
za Tanzania, kinasema “Mtu yeyote aliye kwenye utumishi wa umma ambaye, wakati
akitekeleza majukumu ya ofisi yake akifanya kitendo cha udanganyifu au ukiukaji
dhamana huo ungekuwa ni kosa la jinai kama ungefanywa na mtu binafsi au la,
anafanya kosa na endapo atapatikana na hatia atapata adhabu ya kifungo cha
miaka saba jela.”
Lissu
alisema kwa kutumia vyeti vya shule visivyokuwa vyake, na kwa kutumia majina ya
mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma, mkuu huyo mwenye jina halisi la
Daudi Bashite ameathiri imani ya wananchi kwa serikali yao kwa kuajiri na
kulinda watu wadanganyifu na wasiokuwa na vyeti halali.
“Mtu
huyu amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa mahakamani na
endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za
kawaida za nchi yetu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema).
Lissu
aliongeza kuwa endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakataa kutoa ridhaa, TLS
itamfungulia mkuu huyo wa mkoa mashtaka ya rejea ya kimahakama katika Mahakama
Kuu ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo.
Kabla
ya kumkabidhi Rais Magufuli ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu na kitaluma
kwa watumishi wa umma nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Uatawala
Bora, Angela Kairuki, alisema watumishi 9,932 walikutwa na vyeti vya kughushi
na kwamba, ripoti hiyo haikuwagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu
wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na madiuwani.
Hata
hivyo, Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi, alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha
Sheria ya Utumishi wa Umma namba 3 na 5, tafsiri ya mtumishi wa umma
inawahusisha pia Wakuu wa mikoa na Wakuu wa Wilaya na hivyo kina Bashite
walipaswa pia kuhusishwa katika uhakiki huo.
No comments