Breaking News

TGNP YAWANOA WANAFUNZI WASICHANA WALIOHITIMU NA KUFAULU VIZURI VYUONI

Mtandao wa Wanawake Tanzania (TGNP)  Changamoto kubwa za kielimu zinazowakabili wasichana katika safari ya ufaulu wa masomo ni kubwa ikilinganishwa na wavulana kwakuwa wasichana hubebeshwa majukumu mengi zaidi ambayo hupunguza muda wao wa kujisomea   

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapongeza wasichana 38 waliofanya vizuri katika elimu ya juu, jijini Dar es Salaam Mkurugenzi  Mtendaji wa (TGNP), Bi  Lilian Liundi, alisema wasichana wengi wanashindwa kufikia malengo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kujiingiza katika masuala ya mapenzi wakiwa bado shuleni na kuwa na mtazamo wa kwamba wao ni wanyonge.

Alisema wasichana hawa ambao wamefanya vizuri kutoka katika vyuo mbalimbali pamoja na kuwepo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wameonesha ukombozi kwa wasichana wenzao kwa kuonyesha kuwa wanaweza kuleta maendeleo ya mwanamke mwezio.
Bi Liundi amefafanua kuwa TGNP imekuwa mstari wa mbele katika kuendesha harakati za kumkomboa mwanamke katika changamoto mbalimbali sambamba na kuendesha semina na warsha mbalimbali ambazo zimekuwa zikijikita zaidi katika jitihada za kumkomboa mwanamke sambamba kuwajengea uwezo.

Aidha aliongeza kuwa kuendelea kuwepo na fikra potofu kwa wanawake wengi wamekuwa wakijiona kama wao ni daraja la pili hali ambayo inafanya kukosa haki zao za msingi na kuendelea kuweka mfumo dume wa maamuzi kufanywa na wanaume.


Kwa upande wake Mmoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji, bi Aisha Soudy alisema wasichana wanakabiliana na changamoto nyingi moja wapo ni kuendelea kuwepo kwa mila na tamaduni ambazo humpendelea mtoto wa kiume huku mtoto wa kike akionekana asiyeweza kufanya kitu,

Naye mhitimu aliyefanya vizuri katika matokeo ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Sara Mgonela alisema msichana ana nafasi yake kama  akijitambua anachokifanya katika jamii yake.

Alisema licha ya kuwepo changamoto nyingi kama mtoto wa kike aliweza kufanya vizuri na kuwataka wasichana kujiamini kuwa wanaweza na kuwa na bidii.