Breaking News

TECMN: KUZUIA WATOTO WAKIKE WALIOPATA MIMBA KUENDELEA NA MASOMO KUWANYIMA HAKI YAO YA KUPATA ELIMU BORA

Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania (TECMN) Umeshangazwa na kusikitishwa sana na kitendo cha baadhi ya wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kuunga mkono hoja ya kutowapa wanafunzi wa kike waliopata ujauzito nafasi ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es salaam mwenyekiti wa (TECMN) Bi Valerie Msoka  amesema kuwa kitendo hicho kinarudisha nyuma jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuleta usawa wa kijinjisia na kumuinua mwanamke katika Nyanja zote kijamii, kisiasa na hata kitamaduni.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya kidemografia na afya Tanzania wa mwaka 2015-2016 inaonyesha kuwepo ongezeko la mimba za utotoni kwa asilimia zaidi ya 27 kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ikilinganishwa na asilimia 23 ya mwaka 2010.

Bi Msoka alifafanua kuwa Utafiti huo umeonyesha kuwa sababu kubwa inayopelekea wasichana wengi kupata mimba za utotoni zinazopelekea kukatiza masomo yao ni uelewa mdogo sana wa elimu ya afya ya uzazi ambapo asilimia 50 ya wasichana wenye umri wa miaka 18 hawana kabisa uelewa huo.

“Kitendo cha wabunge kushindwa kuwa na msimamo wa pamoja katika kuishinikiza serikali kuweka mkazo katika kuwasaidia watoto wa kike kuendelea kupata elimu pale watakapokuwa wamepata mimba wakiwa shuleni ni kumnyima mtoto wa kike nafasi ya elimu ni kuomuongezea umaskini, udhalilishwaji wa kijinsia pamoja na kukwamisha jitihada zinazochukuliwa kumkwamua kimaendeleo, kiuchumi, kisiasa na kijamii" Alisema Bi Msoka.

kwa upande wake Mkurugenzi wa chama cha waandishi wanawake tanzania (TAMWA), Bi. EDA SANGA  Amevitaka vyombo vya habari nchini kuzingatia kurusha vipindi  vyenye maadili ili kujenga jamii iliyo Bora sambamba na kuandaa vipindi vitakavyomsaidia mtoto wa kike  kutimiza ndoto  zake.