TANZANIA YASHIKA NAFASI YA TATU AFRIKA KWA SHERIA BORA YA USIMAMIZI NA UDHIBITI WA KEMIKALI
Mkemia
Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu
Tanzania kushika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na Sheria bora ya
Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali hali iliyopelekea Taasisi hiyo kuwa moja ya Taasisi
bora zenye maabara ya kisasa.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora
wa Bidhaa, Daniel Ndiyo na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Biashara, George Kasinga.
Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora wa Bidhaa, Daniel Ndiyo akiwaeleza
waandishi wa habari umuhimu wa wananchi kupata taarifa na maamuzi ya mkutano wa
Kimataifa kuhusu Udhibiti wa kemikali na kemikali taka uliofanyika hivi
karibuni Geneva, Uswisi kuanzia Aprili
24 hadi Mei 5 mwaka huu.
Meneja
wa Kanda ya Kaskazini GCLA, Christopher Anyango akifafanua kuhusu mkakati wa
Serikali kuwajengea uwezo wananchi kuelewa madhara yatokanayo na kemikali
ambazo zimepigwa marufuku.
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Tanzania
imeshika nafasi ya tatu barani Afrika ikiongozwa na nchi ya Afrika Kusini na
Nigeria kwa kuwa na Sheria bora ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali.
Kauli
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA),
Prof. Samweli Manyele alipokua akizungumza na waandishi wa habari juu ya
mkutano wa Kimataifa wa Udhibiti wa Kemikali na Kemikali Taka uliofanyika
Geneva, Uswisi kuanzia Aprili 24 hadi Mei 5 mwaka huu.
Prof.
Manyele amesema kuwa katika Bara la Afrika Tanzania ndio nchi pekee ambayo ina
taasisi ya Serikali inayosimamia kemikali wakati nchi zingine usimamizi wa
masuala ya kemikali upo katika taasisi za mazingira kitu ambacho kinapelekea
usimamizi hafifu wa kemikali hizo.
“Tanzania
ni nchi pekee Afrika ambayo taasisi inayohusika na masuala ya kemikali ipo
chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na pia ni
taasisi yenye kusimamiwa na wataalamu wa kemikali waliobobea pamoja na kuwa na
maabara kubwa inayojulikana kimataifa,”alisema Prof. Manyele.
Akiongelea
kuhusu mkutano huo, Prof. Manyele amesema kushiriki katika mkutano huo ni jambo
la kisheria hivyo kupeleka watumishi watatu kutoka kwenye taasisi hiyo
inadhihirisha kuwa Tanzania imetimiza majukumu yake kama Taifa.
Amefafanua
kuwa mkutano huo unaisaidia taasisi kutoa taarifa kuhusu utendaji kazi,
kujifunza nchi zingine wanafanyaje kazi zao, kupata majibu ya moja kwa moja
pamoja na kujadiliana namna ambavyo wataboresha utendaji kazi.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora wa Bidhaa, Daniel Ndiyo
ametaja wadau wanaotakiwa kupata taarifa na maamuzi ya mkutano huo kuwa ni
wafanyabiashara, watumiaji wa kemikali hizo pamoja na mamlaka mbali mbali za
usimamizi wa kemikali.
Naye
Meneja wa Kanda ya Kaskazini GCLA , Christopher Anyango amesema mkutano huo
unawasaidia wananchi kupata msaada wa haraka kutoka katika Ofisi ya Mkemia Mkuu
wa Serikali kwa kuwa wana uelewa pamoja na kupata mafunzo ya kemikali
zinazoruhusiwa na zisizoruhusiwa kulingana na mahitaji kwa wakati husika.
Maabara
ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilishiriki katika mkutano huo wa utekelezaji wa
mikataba mitatu ikiwemo ya usafirishaji wa taka sumu kimataifa (Basel), mkataba
unaohusu kemikali zenye madhara na zinazochukua muda mrefu kuoza katika
mazingira (Stockholm) pamoja na mkataba wa Rotterdam unaohusu upashanaji
taarifa juu ya kemikali hatari na viuatilifu katika biashara ya kimataifa.
No comments