Breaking News

RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA PROFESA MUHONGO



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo muda mfupi baada ya kupokea ripoti ya Kamati ya kuchunguza mchanga wa madini (makinikia) uliomo kwenye makontena yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini itajazwa baadae.

Mapema asubuhi baada ya kupokea ripoti hiyo iliyoonesha mchanga uliokuwa unachunguzwa ulikuwa na wastani wa kiasi cha thamani kati ya shilingi bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani wa chini na trilioni 1.439 kwa kutumia viwango vya juu.

Kufuatia taarifa hiyo Rais Magufuli aliivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo kutokana na kutosimamia ipasavyo mchakato mzima wa usafirishaji mchanga wenye madini nje ya nchi na hivyo kuisababishia nchi hasara kubwa.

“Nawapongeza Kamati kwa ripoti mliyoiwasilisha ambayo inasikitisha na ripoti hii haiwezi kupita hivi hivi kwani tutaonekana watu wa ajabu".

Hivyo kuanzia sasa nimeivunja rasmi Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), nimemsimamisha kazi Afisa Mtendaji Mkuu wa TMAA pia  namtaka Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ambaye ni rafiki yangu lakini kwenye hili ningependa ajifikirie na achukue hatua ya kujiuzuru”, alieleza Rais Magufuli kabla ya kutengua uteuzi wa Waziri Muhongo.

Mbali na kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati, kuvunja Bodi ya Wakurugenzi na kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa TMAA, Dkt. Magufli pia amevitaka vyombo vya dola kuwachunguza na kuwachukulia hatua watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na wafanyakzi wote waliohusika na kushindwa kusimamia vema mchakato mzima wa usafirishaji wa mchanga wenye madini nje ya nchi.

Akifafanua taarifa ya ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi wa Mchanga wa Madini, Prof. Abdulkarim Mruma amesema kuwa katika uchunguzi huo wamebaini kuwa kuna viwango vikubwa vya madini yanayojulikana pamoja na aina zingine za madini yasizojulikana ambayo ni muhimu na ya gharama ambayo yalikuwa yakichukuliwa bila kuhesabiwa.

“Tumeyafanyia uchunguzi jumla ya makontena 277 ambayo yalizuiliwa kusafirishwa na Mhe. Rais Magufuli kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina hivyo katika uchunguzi wetu tumegundua kuwa makontena 277 yenye madini ya kawaida pamoja madini ya kimkakati thamani yake ni wastani wa bilioni 829.4 hadi trilioni 1.439”, alisema Prof. Mruma.

Prof. Mruma ameongeza kuwa Kamati hiyo imebaini ukosefu wa vifaa vya kukagulia (scanner) vitu vilivyomo kwenye makontena hayo kwani baada ya kufanya ukaguzi vifaa hivyo havikuonyesha vitu vilivyomo ndani.

Machi 29 mwaka huu, Rais Magufuli aliunda Kamati ya kwanza ya watu nane ikiongozwa na Profesa Abdulrahim Mruma kuchunguza makontena 277 yenye mchanga uliokuwa usafirishwe nje ya nchi.