UVCCM IMETOA TAMKO HILI MARA BAADA YA RAIS MAGUFULI KUCHUKUA HATUA SAKATA LA MAKONTENA YA MCHANGA WA MADINI
Ndugu Viongozi na
wanachama wa CCM kwa umoja wetu tumelazimika kukusanyika mahali hapa kwa kazi
moja muhimu ikihusiana na chimbuko la historia ya nchi yetu tokea tulipopata
uhuru Disemba 9 mwaka 1961 na pale yaliofanyika Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Januari 12 mwaka 1964.
Tokea tupate uhuru
Taifa letu lilikumbwa na misukosuko kadhaa ikiwemo mikwamo na mitikisiko ya
kiuchumi.
Kwa bahati nzuri sana
jana Tarehe 24 Mei 2017 limefanyika tukio jingine kubwa la kihistoria ambalo
nalo linalohitaji kuingizwa kwenye kurasa za kumbukumbu muhimu ya nchi yetu.
Tokea tujikomboe,
kuunganishwa kwa mataifa yetu ya Tanganyika na Zanzibar, kujitawala sisi
wenyewe , miaka yote tumekuwa tukihubiri juu ya dhamira ya kuheshimu misingi ya
utaifa na uzalendo.
Viongozi wetu na
maandiko mbalimbali yamehimiza kuhusu matumizi bora ya Rasilimali za Taifa na
Maliasili asili zilizopo. Tumehimizana juu ya kujenga Umoja wa kitaifa,
kupigania haki, usawa, kukataa ukabila na kudumisha amani chini ya Siasa ya
Ujamaa na Kujitegemea.
Katika awamu ya
kwanza ya utawala wa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya
uongozi wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
kulianzishwa Viwanda vingi, kampuni za Serikali na mashirika ya umma.
Nchi yetu ilipiga
hatua kubwa mbele ya mataifa mengine Afrika Mashariki na Afrika kiuchumi kwa
sababu ilimudu kuzalisha bidhaa zake na kuuza ndani na nchi za nje huku ikipata
fedha za kigeni.
Ndugu
Vijana wenzangu
Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hayati Mzee Abeid
Amani Karume, walikuwa na malengo mazuri, mipango na mikakati ya kuzijenga nchi
zao kiuchumi lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watanzania waliokabidhiwa
dhamana za uendeshaji na usimamizi, walipungukiwa na shime ya uzalendo na
kujikuta karakana, Viwanda, Taasisi na Mashirika yalioanzishwa kwa nia njema
yakifilisika.
Hata hivyo
waliohusika katika kufilisi mashirika hayo ya Umma , Viwanda na kampuni za
Serikali kwa namna moja au nyingine, hawakuchukuliwa hatua na wala wahusika
wake kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu jambo lolote.
Pamoja na juhudi
kubwa za uanzishaji wa viwanda na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yakizalisha
bidhaa muhimu,nchi yetu ikajikuta ikirudi hatua nyingi nyuma za kiuchumi na
kimaendeleo kwa sababu ya kukosekana usimamizi makini, uwajibikaji, uwazi na
kutolidhibiti kundi la mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma dhidi ya watu
waliotamani kujivika mataji ya ubepari na unyonyaji.
Hata hivyo
haikushuhudiwa aina ya viongozi walaji Serikalini , wakwapuzi na wabadhirifu wa
mali za umma au mafisadi aidha katika awamu ya kwanza, pili na ya tatu
wakishitakiwa hadi pale kwa mara ya kwanza katika awamu ya nne vigogo watatu
waandamizi wa serikali walipofikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka
kwa kushitakiwa na hukumu kutokewa kwa mujibu wa sharia
Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi unafikiri na kuamini kuwa udhaifu au kulegalega kwa vyombo
husika na dhamana hadi kushindwa kuchukua hatua za kisheria katika kukabiliana
na ubadhirifu wa mali za umma uliofanywa na wezi, wabadhirifu na mafisadi,
kumechangia kwa kiasi kikubwa kulifikisha Taifa letu mahali pabaya kiuchumi
hatimaye hata wanyama kama Twiga na Faru wakipandishwa kwenye ndege kwenda
ughaibuni .
Maendeleo ya kila
Taifa aghalabu hutegemea vyanzo vyake vya ndani kwa maana ya vitega uchumi
vyake, maliasili zake na rasilimali kadhaa ikiwemo mitaji itokanayo na Viwanda,
Mashirika, kampuni za Serikali, wanyama, mbuga, madini, utalii na fursa
nyingine muhimu za kisekta.
Kwa miaka mingi vyanzo
vyote hivyo muhimu vilipokuwa vikizalisha, tija na faida zake zimewanufaisha
watu wachache. Wananchi wengi hasa walioko vijijini wamekuwa wakikosa huduma
bora za kijamii huku familia za wezi na mafisadi zikiishi maisha ya anasa,
fahari na kibwenyenye.
Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi tunadhani kuwa vipindi na zama hizo zimepita na pengine
hazitarudi tena. Sasa kuna zama mpya ambayo ni makini, inayotazama haki na
maslahi ya umma, ikitazama shida za wananchi na kupigania maendeleo yao.
Ndugu
Vijana wenzangu;
Ikumbukwe kuwa tokea
akiwa katika ngwe ya kampeni za kuwaomba ridhaa wananchi ili aliongoze Taifa
letu, Rais Dk John Magufuli aliahidi huku akisema chini ya Serikali yake
itakayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, maliasili na rasilimali zote za nchi
zitawanufaisha wananchi wenyewe na kamwe hazitakwenda katika matumbo na mikono
ya mafisadi na wezi.
Umoja wa Vijana wa
CCM tumeamua kutoka mbele ya hadhara kuelezea kuridhishwa kwetu na hatua
stahiki anazozichukua Rais Magufuli huku akizingatia maelekezo na maagizo
aliyopewa na Chama Cha Mapinduzi kwenda kuyasimamia Serikalini.
Kazi anayoifanya Rais
Magufuli ndiyo kazi tuliyomtuma wana CCM wapenda amani, wazalendo na
wakereketwa wa maendeleo ya Taifa letu la Tanzania.
Hakuna jambo geni na
alilolianzisha mwenyewe Rais Magufuli isipokuwa yote ni maelekezo yanayotokana
na Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015 - 2020.
Wale wanaobeza na
kusema eti CCM kazi yake kufuga wezi tunawaambia wezi, mafisadi, na wala rushwa
CCM sio sehemu yao na ndio maana hawadumu ndani ya Chama na kwenye Serikali
yoyote inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi.
Jambo hili kubwa
alilolifanya Dkt. Magufuli kwa masilahi ya Taifa limezungumzwa na kuwekewa
msisitizo katika Ilani ya Uchaguzi mwaka 2015/2020 nanukuu
(i) “Kusimamia na
kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini ili kukuza
mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa”
(k) “Kubuni na
kutekeleza mikakati mahsusi itakayowezesha kupunguza au kukomesha kabisa
vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya
madini nchini”.
Mapema tarehe 29
March mwaka 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli aliunda Tume ya uchunguzi wa mchanga wa madini ili kujua ni kiasi gani
Taifa linapoteza bila kunufaika. Tume hiyo ikapewa hadidu za rejea ili
kukamilisha kazi hiyo kwa weledi, uwazi na kuipatia serikali majawabu ya
kutosha.
Hivyo kwa maelezo
hayo Umoja wa Vijana wa CCM unaunga mkono ripoti ya Kamati, matokeo ya
uchunguzi na mapendekezo yake hivyo kwa kauli moja Vijana tunatamka ifuatavyo:-
TAMKO
LA UVCCM BAADA YA RIPOTI YA TUME :
• Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi tunampongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa na uzalendo wa hali ya juu alionao kwa Taifa.
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunaunga mkono maamuzi yote yaliyopitishwa au kutolewa na Rais Dk John
Magufuli mara baada ya kupokea ripoti ya Tume ya Uchunguzi
• Umoja wa Vijana wa
CCM hutuko tayari na hatutakubali kushuhudia tena Tanzania ikirejea katika zama
ya kiza kinene cha ukwapuaji mali, ulaji, kufilisi mashirika ya umma au wizi wa
mali za umma.
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunaishauri serikali yetu iendelee na mikakati yake ya kuhakikisha
ukwapuaji, ubabaishaji, wizi na ufisadi wa mali za serikali vinavikomeshwa mara
moja
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunaiomba kwa dhati Serikali yetu ianze kuipitia upya mikataba yote ya
madini ili kubaini kama ni yenye manufaa na maslahi mapana kwa umma .
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunamuomba Rais Dk John Magufuli kuwaweka pembeni wasaidizi wake wote ambao
bado wanaonekana kuwa na kigugumizi katika kuwatumikia wananchi huku baadhi yao
wakiona muhali kupambana na ufisadi.
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunasisitiza kuwa Watendaji wote waliokuwa na dhamana na ambao wamehusika
kwa namna moja au nyingine kupoteza mapato na kulitia hasara Taifa, hatua za
kisheria zichukuliwe dhidi yao haraka .
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunaishauri Serikali kuendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua Viongozi na
watendaji wa serikali ambao watabainika kumiliki mali, utajiri na vitega uchumi
ambavyo havitokani na mapato yasiolingana na vipato vyao wataifishwe kama
ilivyofanyika mwaka 1967 baada ya kutangazwa Azimio la Arusha .
• Umoja wa Vijana wa
CCM tunaishauri serikali kuendesha shughuli zake za kiutawala kwa kusimamia,
kuongozwa na kufuata miiko na maadili ya uongozi kama yalivyotajwa na
kuelekezwa katika Azimio la Arusha kwa sababu Azimio hilo lipo hai kisheria na
bado halijafa.
• Vijana wote
tunaishauri serikali yetu isikubali na isiafiki mali za umma zitumike kwa
maslahi binafsi badala yake kila miliki ya serikali na mali ya umma ifahamike
kuwa kila mwananchi ana haki kufaidika nayo ambayo ni sehemu ya matunda ya
Uhuru na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Aidha Umoja wa Vijana
wa CCM unawataka wana CCM na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kumuunga
mkono Mheshimiwa Rais na Serikali yake katika mapambano dhidi ya vikundi vya
rushwa, ufisadi na uzembe kwa baadhi ya watendaji ili kuleta maendeleo endelevu
katika taifa letu. Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM tunaahidi tutamlinda, tutamtetea
kwa gharama yoyote Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM
kwa kutekeleza mambo yote mema ambayo tunaamini yataleta mabadiliko makubwa ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii. Vijana tumeendelea kuwa na imani kubwa na Ndugu
John Joseph Magufuli kuwa changamoto nyingi za Vijana kumalizakia zinawezekana
kwa kuimarisha Uchumi kwanza ili Vijana waweze kufanya kazi kupitia rasilimali
za nchi yetu.
Wito kwa Vijana
wenzetu hakuna kukata tamaa sasa ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii mwanga
wa matumaini umeonekana sura mpya ya taifa linaweka katika mageuzi makubwa ya
kiuchumi imeonekana.
Mungu Ibariki
Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
KIDUMU CHAMA CHA
MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka
(MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU