MWENGE WAIBUA MZOZO BUNGENI

Serikali
imesema haina mpango wowote wa kusitisha mbio za mwenge wa uhuru na kwamba
dhana ya kutekeleza kitendo hicho kitaendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi
kingine huku ikiahidi kuwa zoezi hilo litasisitizwa bila kuchoka.
Kauli
hiyo imetolewa leo Bungeni na Waziri wa
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama wakati
akijibu swali la Mbunge wa Konde, ndugu Khatib Said Haji aliyekuwa akitaka
kujua faida za kuwasha na kuzungushwa kwa mwenge nchi nzima na kama hakuna kwa
nini zoezi hilo lisifutwe.
Waziri
Mhagama ameendelea kufafanua kwamba Mwenge umesaidia sana katika kukuza ari za
maendeleo katika nchi ikiwa ni pamoja na uwekwaji wa mawe ya msingi katika
miradi inayoandaliwa na wananchi huku ukiendelea kuhamasisha uzalendo pamoja na
umoja ikiwa ni ishara ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.
"Mtanzania
yoyote anayemuenzi baba wa Taifa hili halafu akaukataa Mwenge wa uhuru itabidi
tumshangae kwa sababu yeye ndiye muasisi na aliuwasha akiwa ana nia umulike
wanyang'anyi, wezi lakini pia uangaze maendeleo, kudumisha amani na mshikamano.
Mwenge wa uhuru ni tunu kubwa katika uhuru wa nchi yetu hivyo ni wajibu wa kila
mtanzania kuuheshimu mwenge" Mhagama alisisitiza.
Pamoja
na hayo Waziri Mhagama amefafanua na kuweka wazi pamoja na dosari ndogo ndogo
zinazojitokeza wakati wa ukimbizwaji wa mwenge hazitakuwa chanzo cha kusitisha
zoezi hilo bali zitatafutiwa ufumbuzi.
"Dosari
ndogo ndogo zinazojitokeza tutazitafutia ufumbuzi lakini siyo kusitisha zoezi
la kukimbiza mwenge. Mwenge huu wa uhuru utadumu na utakuwa kama chachu ya
maendeleao nchini" aliongeza Mh. Mhagama.
No comments