Breaking News

MWALIMU MKUU ASIMULIA AJALI ILIYOUA WANAFUNZI 32


Wakazi wa Rhotia, wilayani Karatu mkoani Arusha wakitazama basi dogo lililokuwa limebeba wanafunzi wa Shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vicent ya jijini Arusha baada ya kutumbukia kwenye korongo la Mto Marera, Kata ya Rhotia jana.

Karatu
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Lucky Vicent Academy waliyokuwa wanasoma wanafunzi 32 waliofariki dunia kwa ajali jana, Longino Vicent amesema ndiye aliyesimamia safari iliyosababisha vifo vya watoto hao na wafanyakazi watatu.

Vicent amesema wanafunzi hao na walimu wawili pamoja na dereva waliofariki, walianza safari yao saa 12:30 asubuhi kuelekea Karatu ambako watoto hao walipaswa kufanya mtihani wa kujipima uwezo na wale wa Shule ya Tumaini.

“Mimi ndiye niliyesimamia safari hiyo na niliwasafirisha waliondoka hapa saa 12; 30 asubuhi, sikufikiri kama yatatokea haya. Kila kitu kilikuwa salama tu,” alisema akisimulia walivyoanza safari watoto hao kabla ya gari walilopanda aina ya Toyota Costa lenye namba za usajili T 871 BYS kupinduka korongoni na kusababisha vifo hivyo.

Mwalimu Longino alisema shule hizo mbili zimekuwa na tabia ya kufanya mitihani ya ujirani mwema na kuwa hiyo ni mara ya tatu.
“Huu ni mwaka wa tatu, hata shule ya Tumaini huwa inakuja Arusha,” alisema.

Mwalimu huyo alisema shule hiyo ilikuwa ya kwanza kimkoa mwaka 2004 na ya 20 kimkoa katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana.

Wanafunzi hao waliofariki dunia walikuwa wakisoma shule hiyo ya bweni ambayo kwa mujibu wa wakazi wa Arusha ni miongoni mwa shule bora na iliyotoa mwanafunzi bora katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alisema eneo la ajali lina kona nyingi na mteremko mkali na kwamba, kuna maeneo ambayo yamekuwa yakisababisha ajali kutokana na miundombinu yake ilivyokaa.

Aliyataja eneo jingine kuwa lipo barabara ya Morogoro kwenda Dodoma linaloitwa Makunganya lina utelezi mwingi na kuwasihi madereva kuwa makini sana wakati wa mvua. Wanafunzi waliofariki ni wa darasa la saba.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro alisema miili ya wanafunzi hao itaagwa katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid leo.

No comments