MEYA MTINIKA: WANANCHI TUMIENI NISHATI SAFI ZA KUPIKIA YA BRIQUETTES
Meya wa Manispaa ya Temeke mheshimiwa, Abdallah Mtinika amesema matumizi ya mkaa Rafiki Briquettes umekuja kuondoa na kutokomeza matumizi ya Nishati Chafu ambayo sio rafiki kwa Afya kwa wanaotumia nishati hiyo.
Akizungumza katika Kilele cha wiki ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na Rafiki ya Briquettes kwa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Mtinike amesema, ukikuta mtu ameletewa nishati safi na rahisi kama mkaa huu na bado anatumia nishati chafu basi huyo hana tofauti na mchawi.
Alisema na kurejea agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kwamba mpaka mwisho wa mwaka huu kila taasisi yenye kuhudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia na tayali Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imejipanga kufanya ukaguzi kwa lengo la kuona utekelezaji wa agizo hilo.
Mhe. Mtinika amewataka Wananchi hususani wa Wilaya ya Temeke kuchangamkia fursa na kuiamini nishati hiyo na kuanza kuitumia na kuachana na matumizi yasiyofaa ya Nishati chafu.
Amewapongeza kinamama katika makundi mbalimbali kama chama cha Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Chama cha Wanawake Tanzania (CHAWATA) na vinginevyo kwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa Nishati Safi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dokta. Venance Mwasse amesema nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes ni Mkombozi katika mapambano dhidi ya nishati Chafu na kwamba Nishati hiyo ni mkombozi kwa Watanzania.
Amesema Nishati hiyo ambayo ni mkaa unaotokana na makaa ya mawe umefanyiwa utafiti na vyuo vikuu mbalimbali na kubainika kuwa unakidhi mahitaji ya watanzania kwani ni rafiki na bidhaa hiyo ni bei nafuu.
Aidha, aliongeza kuwa STAMICO tayari wamesimika mitambo mikubwa ya kuzalisha mkaa huo kwenye Wilaya za Kisarawe mkoani Pwani na Kyela mkoani Mbeya kunakozalisha makaa ya mawe ambapo uzalishaji kwa sasa umefikia Tani elfu ishirini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Usimamizi wa Majiko kutoka Jeshi la Magereza mkoa wa Dar es Salaam, Sajenti Yohana Simwenda amesema Nishati Safi ya Kupikia ya Rafiki Briquettes imelisaidia Jeshi hilo kuokoa fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kuokoa miti ambayo wangeikata kama kuni za kupikia.
Amesema mkaa huo unauwezo wa kupikia vyakula vingi bila kuongeza mwingine huku akisema Gereza moja lenye watu zaidi ya 1000 wanaweza kupikia kilo 19 kwa vyakula vyote na bado ukabaki.
"Jeshi la magereza linatoa shukran kwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa kuwarahisishia Magereza kuwa hawapati tena tabu ya kutafuta kuni". Alisema Sajenti Simwenda
No comments