MTIKISIKO WA UCHUMI: BENKI 3 HATARINI KUFUNGWA

Hali ya mtikisiko wa
uchumi uliozikumba taasisi nyingi, hasa za fedha sasa unazinyemelea benki tatu
ambazo zinaweza kuwekwa chini ya uangalizi maalumu wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kama ilivyokuwa kwa Twiga Bancorp.
Twiga Bancorp, ambayo
kwa sehemu kubwa inamilikiwa na Serikali, imewekwa chini ya uangalizi wa BoT
baada ya madeni yasiyolipwa (NPL) kuzidi kiwango kinachotakiwa kisheria.
Hali hiyo
inazinyemelea taasisi nyingine tatu za fedha Benki ya Wanawake (TWB), ambayo
pia inamilikiwa na Serikali, Ecobank Tanzania na Efatha Bank, ambayo
inahusishwa na taasisi ya kidini ya Efatha, kwa mujibu wa uchambuzi wa The
Citizen
Benki hizo tatu
zimelimbikiza kiwango cha NPL kinachozidi asilimia 50 ya jumla ya mikopo
iliyotolewa, huku kiwango cha Efatha kikifikia asilimia 63.
Wataalamu wa benki
wanaamini kuwa kiwango cha NPL kinachozidi asilimia 15 ya jumla ya mikopo yote
ya beki za biashara, kinaashiria uwezekano wa kuanguka.
Katika toleo la tisa
la Hali ya Kiuchumi Tanzania, Benki ya Dunia ilitahadharisha kuhusu kukua
kupita kiasi kwa kiwango cha NPL, ambacho kilifikia asilimia 9.5 mwaka 2016
kutoka asilimia 6.4 mwaka 2015.
Ripoti hiyo iliitaja
TIB Development Bank ambayo kiwango chake cha NPL kilikuwa asilimia 38 katika
robo ya kwanza ya mwaka 2017.
Hata hivyo, taarifa
za fedha za benki za biashara za robo ya kwanza mwaka 2017 zinaonyesha hali ni
mbaya zaidi kwa Efatha, TWB na Ecobank Tanzania.
No comments