MEYA WA JIJI ISAYA MWITA ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MRADI OCEAN ROAD.
NA CHRISTINA MWAGALA,(OMJ)
, Dar es Salaam.
MEYA wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita ameridhishwa na kasi
ya ujenzi wa mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na
maboresho ya maeneo ya umma katika fukwe ya Ocean Road.
Mradi huo ambao unatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka
huu, utakuwa ni mahususi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa ajili kutunza
mazingira na kuepukana na mafuriko.
Alifafanua kwamba, mradi huo utahusisha ujenzi wa
vyoo na mabenchi ya kupumzikia, utakuwa na jumla ya urefu wa mita 860 kuanzia
Hospitali ya Agha-Khani kupitia viwanja vya Ikulu.
“Ukiangalia kwenye fukwe zetu hazina vyoo, hivyo
kuwafanya watu wanaokuja kupumzika kukosa sehemu za kwenda kujihifadhi, jambo
ambalo sio zuri, ukizingatia jiji letu linapokea wageni kutoka sehemu
mbalimbali, ndio maana tumeamua kuleta mradi huu ili kuondoa aibu hii”
alifafanua
Katika ziara hiyo iliyofanyika
hivi karibuni, Meya alisema kwamba maeneo ya kupumzikia katika jiji la Dar es
Salaam sio rafiki kutokana na ukosefu wa miundombinu hivyo kukamilika kwa mradi
huu kutaondoa baadhi ya changamoto zilizopo kwenye maeneo ya hayo.
“Jiji letu ukiangalia kimiundombinu haliko vizuri,
mpangilio wake pia hauko vizuri, sasa inapotokea mabadiliko yoyote, wananchi
hujikuta kwenye athari kubwa sana, hivyo kupitia mradi huu, utaondoa changamoto
hizi” alisema Meya.
“ Ukienda kwenye majiji mengine,
utakuta sehemu za fukwe kama hizi , watu wanapumzika, lakini pia ni chanzo cha
mapato kwa jiji kwa sababu wanalipia, ila kwetu hapa, imekuwa ni jambo la
kawaida, watu wakuja kupumzika kiholela, huu ndio muda wetu wa kulibadilisha
jiji letu la Dar es Salaam” aliongeza.
Akizungumzia vikundi mbalimbali ambavyo vilipewa
mikopo kwa ajili ya kujiendeleza, Meya Isaya alisisitiza kwamba, bado nafasi
zipo kwa vikundi vingine vinavyohitaji mikopo kwa masharti ya uaminifu.
Alifafanua kwamba vikundi vyote ambavyo vitakidhi
vigezo, vitapewa mikopo na kwamba lengo kubwa ni kuwakwamua wananchi kiuchumi
kupitia vikundi ambavyo vimeamua kujitoa kwa ajili ya kupambana na umasikini.
No comments