MAALIM SEIF: LIPUMBA HANA UWEZO WA KUNIVUA UKATIBU MKUU CUF
![]() |
Sarakasi
za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu Mkuu
wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa
kukihujumu chama hicho.
Maalim
Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na
ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa anakihujumu chama ili kishindwe
kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi.
Aliyasema
hayo jana katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipozungumza na
wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya uimarishaji wa chama katika
mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.
Maalim
Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu kutoka vyombo vya dola na
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu chama hicho, lakini
hawataweza kufikia malengo hayo.
Alisema
taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono Lipumba kwa kumpa kila nguvu
anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM ya kuitawala nchi bila ya
kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao hizo zitagonga mwamba.
“Nashangaa
sana kuona Lipumba amekubali kutumika na CCM kwa kukihujumu chama kwa masilahi
binafsi, lakini nataka muelewe wananchi kuwa pamoja na nguvu zao zote hizo katu
hawataweza kuwakatisha tamaa Wazanzibari ya kudai haki yao waliyoipata katika
uchaguzi uliopita,” alisema.
Alishangazwa
kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo vya dola badala ya kufuata
Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.
“Pamoja
na hujuma hizi zinazofanywa na Lipumba katika chama chetu, lakini nashangaa
Rais (John) Magufuli anatumbua watendaji wabovu, lakini humu mrajisi (Msajili)
wa Vyama vya Siasa anamuachia,” alisema.
Kuhusu
kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF,
Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama angekuwa ni mwenyekiti
halali.
Alisema
kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake lazima mkutano mkuu
uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.
Alisema
kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba kilihudhuriwa na wajumbe
wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa kuonesha kama kikao hicho
kilikuwa halali.
“Ikiwa
mimi nimefukuzwa chama kutokana na madai kuwa sihudhurii vikao vinavyofanywa na
ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam, mbona yeye Lipumba tangu mwaka 2015
hawajawahi kuja ofisi kuu ya chama ambayo ni mtendeni hadi leo, kwa hiyo naye
alitakiwa kufukuzwa,” alihoji.
Maalim
Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo yaliyofanywa na Lipumba kwa
kushirikiana na wajumbe wake.
“Ninachokifahamu
mimi ndani ya katiba yetu inasema kuwa ili uamuzi wa kuvuliwa nafasi ya uongozi
ni lazima anayedaiwa kufanya kosa aitwe na uongozi kujieleza, lakini mimi
sijaitwa kujieleza,” alihoji Maalim Seif.
Akizungumzia
madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alisema waliwataka
wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku akidai hivi karibuni dola
ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uongozi wa CUF
unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau
wajibu wao.
Alisema
kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya wanachama na viongozi wake,
lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa vyombo hivyo kuwa ni miongoni mwa
wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.
Alisema
pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama hicho chini ya Maalim
Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.
Akijibu
tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na anayemuunga mkono Profesa
Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa ndiye anakula njama za
kukidhoofisha chama.
Alisema
Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna mikutano na hakuna hata
pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa chama kikuu cha upinzani
kutokana na kuwa wamoja.
“Malalamiko
anayotoa ajikite kwenye katiba, aichambue kifungu kwa kifungu atabaini anakosea
wapi.
“Hii
ni taasisi ya chama, siyo kampuni ya
mtu, lazima tufuate katiba tuliyojiwekea ambayo ipo wazi inatoa maelekezo ya
kila kitu, anayekengeuka anafanya makusudi na sisi hatuwezi kukaa kimya bila
kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteua watakaofanya kazi alizotakiwa kufanya
yeye,” alisema Sakaya.
Alieleza
kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na anatumiwa kufanya hivyo
akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Amekuwa
bwana kesi, kila kukicha anafungua mpya, mimi nina kesi, Lipumba ana kesi,
Msajili wa Vyama ana kesi, mwanasheria ana kesi, akae kimya asubiri ziishe,
”alisema Naibu katibu mkuu huyo.
|
No comments