KUFATIA KUWEPO MADAI YA DK. SLAA KUTAKA KUJIUNGA NA CUF, HII NDIO KAULI YAKE.
Wakati mgogoro
ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukizidi kutokota, Mwenyekiti anayetambuliwa
na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba anadaiwa
kutaka kumvuta aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Dk. Wilbroad Slaa, kujiunga na CUF.
Madai hayo
yameibuka baada ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya Prof. Lipumba na
Dk. Slaa ambao kwa nyakati tofauti mwaka 2015, walijiondoa kwenye vyama vyao
kipindi cha mchakato wa kusaka mgombea urais wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya wananchi (Ukawa).
Ingawa Dk. Slaa
katika mahojiano alikanusha habari za yeye kutaka kujiunga na CUF, lakini habari
zinasema kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba amekuwa akihaha kumshawishi Dk.
Slaa pindi atakaporejea nchini ajiunge na CUF na kushika moja ya nafasi za juu
za uongozi.
Taarifa za
kuaminika zilieleza kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba na DK. Slaa
yanalenga kuboresha safu ya uongozi wa chama hicho kwa kumpa wadhifa wa Ukatibu
Mkuu au Umakamu Mwenyekiti licha ya kudaiwa kwenda kinyume cha Katiba
iliyoanzisha CUF.
Kwa mujibu wa
katiba hiyo, nafasi za juu za uongozi wa chama hicho zinatakiwa kuzingatia
uwiano wa pande mbili za Muungano. Endapo mwenyekiti anatoka Bara, Katibu Mkuu
atatoka upande wa pili wa Muungano.
Baadhi ya wana CUF
wanaomuunga mkono Prof Lipumba wamekiri kuwa kumekuwa na mawasiliano ya wawili
hao, huku wakisema hakuna anayejua kiini cha kuimarika kwa mawasiliano hayo
wakati huu ambapo CUF imepasuka katika makundi mawili, moja likiongozwa na
Katibu Mkuu Maalim Seif na jingine lipo chini ya Lipumba.
Msemaji wa CUF
inayoongozwa na Maalim Seif, Mbarala Maharagande, amesema kuwa taarifa za
kurudi kwa Dk. Slaa amezisikia japo hajui atajiunga na chama gani.
“Labda wale watu wa Lipumba
ukiwauliza wanaweza kukuhakikishia hilo. Kwa nafasi ya katibu itakuwa ngumu kwa
sababu katiba yetu hairuhusu, lakini kuwa mwanachama anaweza. Nguvu ya Lipumba
ilishapungua sana na wenye chama chao (wananchi) watakwenda kukichukua na
kumtoa ofisini kwa hiyo kama anarudi Dk. Slaa kuja kuongezea nguvu upande huo
inawezekana”. alisema
Maharagande.
Akizungumza kwa
njia ya simu, Dk Slaa aliyekuwa Mbunge wa Karatu alisema taarifa hizo si sahihi
kwani alishaahidi kwamba hatarudi kwenye siasa za vyama.
Alisema hawezi
kuyumba kwenye uamuzi wake licha ya kukataa kuweka wazi kwamba ni lini
atarejeea nchini, alisisitiza kuwa msimamo wake wa kuachana na siasa za vyama
uko palepale.
“Maneno yangu hayayumbi, sitafanya
siasa za vyama, nimeachana nazo. Naomba msiniingize kwenye siasa uchwara,
sizifanyi hizo… Saisa ni ajenda. Hizo siasa za kishabiki zifanyeni nyinyi huko
Tanzania, mimi sifanyi ushabiki, hakuna mtu anayekula ushabiki, ndiyo maana
siasa zangu siku zote ni ajenda, Watu wanataka maji, wanataka chakula, wanataka
elimu bora, si ushabiki”
“Kwa miaka 20 niliyokuwa kwenye siasa
sijawahi kufanya ushabiki, nilitafuta ajenda na kuipanga mikakati kwa
ajili ya wananchi” alisema Dk
Slaa alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema atasimama
kupiga kelele kwa ajili ya Tanzania pale atakapoona mambo yanakwenda kombo na
atafanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa si siasa.
Septemba 25, 2015
akizungumza na wandishi wa habari kwa zaidi ya saa 2 kisha kutangaza kujitoa
Chadema, alisema ni afadhali apotee kwenye ulimwengu wa siasa duniani kuliko
kumuunga mkono Lowassa.
Credit:
TanzaniaDaima
No comments