KAULI YA CCM KWA MAKADA WANAOLALAMIKA BAADA YA KUTUMBULIWA NA RAIS
Chama cha Mapinduzi
(CCM) kimeibuka na kukemea vikali kauli zinazotolewa na viongozi au makada wa
chama hicho wambao wametenguliwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika nafasi
zao mbalimbali walizokuwa wakishikilia.
Katibu wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu
Ngemela Lubinga aliyasema hayo juzi akizungumza Mjini Iringa katika mkutano na
wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyomo mkoani humo ambao ni wananchama na pia
viongozi wa chama hicho katika ngazi ya matawi na kata.
Lubinga aliwataka
makada hao walioteuliwa na kisha kutemwa na Rais Dkt Mwagufuli ambaye pia ni
Mwenyeketi wa CCM Taifa, kuacha kulalamika na kupiga kelele badala yake
wakubiliane na mabadiliko hayo kwa nia ya kuheshimu maamuzi ya Ikulu kwa uamuzi
uliochukuliwa dhidi yao.
Licha ya kuwa
kiongozi huyo hakutaja majina ya viongozi aliowataka kuheshimu maamuzi ya
Ikulu, lakini ni dhahiri kuwa miongoni mwa waliolengwa ni Mbunge wa Mtama
(CCM), Nape Moses Nnauye ambaye alitenguliwa katika nafasi yake aliyokuwa ya
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nafasi aliyoitumikia kwa kipindi
cha miezi 15.
Nape alitenguliwa
katika nafasi hiyo ikiwa ni saa chache tu tangu alipopokea ripoti ya kuvamiwa
kwa kituo cha Clouds Media Group ambapo ripoti hiyo ilithibitisha kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam ndiye aliyehusika katika tukio hilo.
Nafasi ya Nape
ilichukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison George
Mwakyembe ambaye naye nafasi yake ikajazwa na Mbunge wa kuteuliwa na Rais,
Prof. Palamagamba Aidan John Kabudi ambaye ni mbobezi katika taaluma ya sheria.
Mwingine ambaye
licha ya kuwa hakuenguliwa na Rais moja kwa moja lakini alionyesha
kutoridhishwa na mchakato wa kuenguliwa kwake ndani ya CCM ni aliyekuwa Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji. Yeye alienguliwa alipotaka
kugombea kwa mara ya pili, na tangu hapo amekuwa akilalamika kwa madai
kuwa njia zilizotumika hazikuwa za haki.
“Rais anapoteua kiongozi na kumpa
dhamana ni kwamba anaona kuwa unahitajika, lakini inapofika mahali amekuondoa
ujue mazingira yale huwezi kuyamudu na anakuokoa ili usipate laana. Baadhi ya
viongozi wameondolewa madarakani, lakini wamebaki wakilalamika mitaani
ovyo.” alisema
Kanali Lubinga.
Lubinga alisema
kuwa chama hicho sasa kimejikita kuhakikisha kuwa kinarejesha nidhamu na
uwajibikaji ndani ya chama na serikali ili viongozi wote waliochaguliwa na
kuteuliwa wafanye kazi kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi.
|
No comments