BINTI ANAYEDAIWA KUFA PAPO HAPO JANA TANGI BOVU JIJINI DAR KWA KUGONGWA APATIKANA MAKABURINI LEO HAI
Kijana dereva wa bodaboda, ambaye pia ni mganga wa
jadi, Anuary Abdallah akiwa na binti aliyedaiwa kugongwa na gari kisha kufariki
dunia papo hapo na mwili wake kupelekwa hospitali ya Mwananyamala, na baadaye
kukutwa makaburini akiwa hai akiwa hawezi kuzungumza.
Baadhi ya wananchi wakimshangaa binti huyo huku
wakimshika kujiridhisha kama ni mwenyewe.
Binti huyo akiwa na mama yake mzazi na waganga waliomsaidia
hadi hadi kufikia hatua hiyo.
BINTI anayejulikana kwa jina la Anna Mathew
(18), mkazi wa Mbezi Juu, eneo la Gold Star Jijini Dar es Salaam, aliyedaiwa
kugongwa na gari na kufariki dunia papo hapo eneo la Tangi Bovu Barabara ya
Bagamoyo, majira ya saa 11 alfariji wakati akitokea katika starehe usiku wa
kuamkia Jumatatu ya pasaka ameonekana makaburini akiwa hai.
Habari za binti huyo kufariki zilifika kwa
familia yake kutoka kwa mwendesha Bodaboda mmoja aliyeshuhudia ajali hiyo na
kumtambua marehemu huyo ambaye alisema gari iliyomgonga haikusimama.
Wakisimulia zaidi mashuhuda wa tukio hilo
lililowashangaza wengi walisema baada ya ajali walimfunika na khanga yake
ilIyokuwa katika mkoba wake huku wakisubiri askari kufika eneo la tukio kwa
ajili ya taratibu pamoja na kuchukua mwili.
''Majira
ya saa kumi na mbili walifika polisi na kuchukua mwili huo kisha kuupeleka
hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuhifadhiwa na kusubiri taratibu za
maziko'',alisema
shuhuda mmoja.
Alisema baada ya wanafamilia kupata taarifa
hizo walijikusanya na kwenda hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya
kujiridhisha na kuutambua mwili.
Akizungumzia tukio hilo mama mkubwa wa Anna,
aliyejitambulisha kwa jina la Ester Joseph alisema walipofika hospitalini hapo
alishindwa kuitambua maiti iliyodaiwa ni ya binti yao kutokana na mwili huo
kuvimba.
''Polisi tuliokuwa tumeongozana
nao walianza kunifokea kwamba inakuwaje nashindwa kumtambua mwanangu? Mimi kwa
kweli nilikuwa hata simuelewi vizuri sikuweza kumtambua kwani alikuwa amevimba
uso, hadi askari walianza kunifokea hivyo nikatoka nje lakini alipokwenda baba
yake mzazi alimtambua na kutoa jibu kwamba aliyemuona ndiye hasa mwanawe na
alipoulizwa alisema kuwa alimtambua kupitia miguu'',alisema Ester.
''Baba
mzazi na kaka wa Anna walipoingia walimtambua na kuthibitisha kuwa waliyemuona
mahala hapo alikuwa ni Anna, kisha tukaondoka kurudi nyumbani kuendelea na
taratibu na maandalizi ya maziko, ambapo ilipangwa azikwe leo Jumanne",aliongeza.
Kama ilivyo kawaida ya msiba majirani
walikusanyika na kufanya taratibu zinazotakiwa kufanywa ikiwa ni pamoja na
kuchangisha fedha kwa ajili ya matumizi katika msiba huo,huku wengine wakifunga
Maturubai na akina mama wakiwasha moto kuandaa chakula.
Majira ya jioni majirani walikusanyika kama
ilivyo kawaida ya msiba mara alifika kijana mmoja msibani hapo aliyetambuliwa
kwa jina la Anuary ambaye ni dereva wa bodaboda na pia ni mganga wa jadi ambaye
hafahamiki zaidi kwa kazi hiyo mtaani hapo.
Wakisimulia majirani walisema kuwa kijana huyo
alipofika alianza kupaza sauti na kuwataka majirani kutawanyika kwamba hapakuwa
na msiba mahala hapo na kuwataka kutokula chakula cha msiba.
Kijana
huyo aliteua wazee wawili waliotajwa kwa majina, Mzee Super na Abdallah Mlali,
ili waondoke wote kuelekea alipo binti huyo aliyewekewa matanga kuwa amefariki.
Imeelezwa kuwa baadhi ya watu walianza
kumpinga na kumdharau wakidhani kuwa alikuwa amelewa na akitania, huku wengine
wakimfukuza msibani hapo.
Kijana huyo aliondoka na mzee mmoja kati ya
hao waili, Mzee Super na kwenda naye hadi makaburini ambako walimkuta Anna
akiwa hawezi hata kuzungumza na kijana huyo alipandisha Mashetani na kuanza
kumfuata binti huyo na kumkamata na kisha kuondoka naye hadi katika nyumba ya
jirani na msiba huo.
Baada ya kufika naye Mzee Super alikimbia
kwenda kutoa taarifa kwa wanandugu kuwa binti yao ameonekana akiwa mzima, jambo
ambalo liliwashangaza wanandugu na kuzuka taharuki kubwa mahala hapo huku kila
mmoja akiwa haamini kinachosemwa, baadhi ya ndugu waliondoka na kwenda
kuthibitisha na kumkuta akiwa na mganga huyo huku akiwa hawezi kuzungumza.
Wanandugu walirudi nyumbani na kukaa kikao
huku wakiwa bado hawaamini kile walichokiona wakifananisha na sura ya mwili
waliuona chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mwananyamala.
Baada ya tukio hilo wanandugu walikubaliana na
kumwachia kijana huyo aendelee na kazi ya kumzindua, huku akiwa amepandisha
mashetani na baadaye aliomba kwa wananchi waliokuwa wamefurika nje ya nyumba
hiyo kumletea kuku mweupe ama mwekundu, jambo lililotekelezwa kwa haraka na
majirani hao ambapo dereva mmoja wa bodaboda alijitolea kumfuata kuku wake Goba
na kumleta mahala hapo ili binti afanyiwe dawa hiyo.
Hatimaye Binti alizinduka na kuanza kuongea
huku akiwatambua baadhi ya watu akiwemo mama yake mzazi, Elizabeth Joseph,
akimkumbatia huku akibugujikwa na machozi, shangwe nderemo na vifijo vikitawala
mahala hapo, kutoka kwa wananchi waliofurika eneo hilo na kila mmoja akisema
yake.
''Wanga wa Mbezi Juu mmeshindwa leo, mlizoea
kutufanya mandondocha na kutuulia ndugu zetu leo mmekutana na mbabe wenu''
walisikika baadhi ya wananchi wakisema kwa sauti.
Akizungumza na mtandao huu baada ya kazi hiyo
nzito, Kijana Anuary alisema baada ya kupata taarifa ya msiba huo, aliamua
kumpigia simu babu yake anayeishi jijini Tanga na kumfahamisha mlolongo mzima
wa tukio, lakini babu yake alimwambia kuwa hapakuwa na msiba na wala binti huyo
hajafariki na kumpa maelekezo jinsi ya kumpata akiwa hai.
Alisema na ndipo alipata ujasiri baada ya
maelekezo hayo aliyafanyia kazi, kama alivyowahi kufanya siku za nyuma mtaani
hapo na kufanikisha kumkamata mzee aliyekuwa akiwatesa wakazi wa mtaa huo kwa
kuwalawiti kimazingara, ambaye aliamua kuhama na kukimbia nyumba yake kwa aibu,
kutokana na jinsi alivyokuwa akiogopwa mtaani hapo.
Akisimulia mkasa huo baada ya tukio hilo, Anna
alisema kuwa siku ya sikukuu ya Pasaka, aliondoka nyumbani kwao majira ya jioni
kuelekea katika 'Birthday' ya rafiki yake akiwa na rafiki yake aliyemtaja kwa
jina la Salma.
Alisema
baada ya kumalizika kwa sherehe hiyo walirejea nyumbani na mwenzake ambaye
aliingia ndani na yeye kuingia chooni kujisaidia na wakati akiwa chooni,
alisikia sauti ikimuita jina lake na akaitika akijua aliyekuwa akimwita ni
Salma, ambapo alisema kuwa baada ya hapo hakujua tena kinachoendelea hadi
asubuhi alipojikuta akiwa makaburini.
''Nilipokuwa makaburini, nilikuwa nikiwaona
watu ninaowajua, ndugu zangu wakipita lakini nilikuwa ninawaita wao hawanisikii
wala hawanioni, nilikuwa hata sijielewi hata nielekee wapi wala hata njia ya
kutoka pale siioni, na hadi najikuta hapa nikiwa nimezungukwa na watu kama
hivi'' ,alisema Anna.
Naye kijana aliyeshuhudia ajali hiyo alisema
alishtushwa na taarifa hizo za kuonekana binti huyo akiwa mzima kwani
alishuhudia binti huyo akifunikwa khanga yake mwenyewe na kubebwa na gari
la polisi akiwa amefariki.
Picha Zote na Muhidin Sufiani (MAFOTO)
No comments