ASKOFU: RAIS MAGUFULI MAJIPU UNAYOYATUMBUA NI MAJIPU MADOGO MADOGO...
Rais wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli jana
Sikukuu ya Pasaka, waliungana na Waumini wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania
Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada
hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba Askofu Charles Salalah
aliongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza
majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na alimpongeza kwa kazi kubwa ya
kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia
madaraka yao vibaya na kufuja mali za umma.
“Mhe. Rais
unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua wewe ni majipu
madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za mwanadamu, na jipu
hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi Wakristo wenzako na waumini
wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono katika kazi hii nzito ya kutumbua
majipu haya madogomadogo ya watumishi hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na
mengine mengi” alisema Askofu Charles Salalah.
Akizungumza
katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli aliwashukuru Wakristo wa Kanisa la Africa
Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa kuendelea kumuombea na
ameomba maombi hayo yaendelee, na pia waiombee nchi iendelee kuwa na amani,
umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.
source malunde blog
No comments