Breaking News

WACHIMBAJI, WAUZAJI NA WASAFIRISHAJI WADOGO WA MADINI, WAMWOMBA RAIS MAGUFULI KUONDOA ZUIO LA KUSAFIRISHA MCHANGA WENYE MADINI,


Wachimbaji, wauzaji na wasafirishaji wadogo wa madini, wamemwomba Rais Dk. John Magufuli kuondoa zuio la kusafirisha mchanga wenye madini alilolitoa wiki iliyopita, baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam.

Pia wachimbaji hao wamesikitishwa na hatua ya watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, kumpotosha Rais kuwa makontena yaliyozuiwa bandarini yana mchanga wa dhahabu, badala ya mchanga wenye madini mengine, ikiwa ni pamoja na shaba, chuma, salfa, mercury na nickel.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kiongozi wa wachimbaji wa madini ya nickel kutoka Dodoma, Thobias Rweyemamu, alisema tangu Machi 2, mwaka huu walizuiwa kusafirisha mchanga na mawe jambo ambalo limewasababishia hasara kubwa.

Alisema hata shughuli za uzalishaji katika maeneo ya machimbo zimesimama na kusababisha hasara ya Sh milioni 4 kila siku.

“Tunapata hasara kubwa tangu Machi 2, tunapoteza Sh milioni 4 kila siku, wachimbaji waliokuwa wanaendelea na shughuli zao wamesimama, hali imekuwa ngumu, tutashindwa kuendesha maisha, familia zetu zinatutegemea na kundi kubwa la vijana migodini… hali hii ikiendelea tutawafanyaje?” alihoji Rweyemamu.

Alisema hadi sasa wachimbaji wadogo zaidi ya 110 wamezuiliwa, huku mchanga wenye nickel zaidi ya makontena 60 na copper makontena saba yakiwa na mchanganyiko wa madini yamezuiliwa.

Rweyemamu alisema kutokana na hali hiyo, bado wanaingia hasara ya kulipia ushuru wa Dola za Marekani 20 kila siku ambazo ni  sawa na Dola 12,000 kwa mwezi jambo linalowatia gharama kubwa.

Alisema wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa miaka mingi, baada ya kupata vibali halali kutoka Wizara ya Nishati na Madini na wapo kihalali si kama ilivyoelezwa.

Mchimbaji mwingine, Paul Kaliyemba, alisema Rais Magufuli alipotoa agizo hilo, hawakupaswa kuchanganywa na maelezo ya wataalamu wa wizara.

Kaliyemba alisema wanafanya biashara hiyo kihalali, hata wizara inatambua kwa sababu leseni zilitolewa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na  walifanya ukaguzi na kujiridhisha.

Alisema kutokana na hali hiyo, wamemwandikia barua Rais Magufuli kupitia Wizara ya Nishati na Waziri Mkuu kupitia upya uamuzi wao na wachimbaji wadogo waruhusiwe kuendelea na biashara yao.

Kuibuka kwa wachimbaji hao, kumetokana na Rais Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye madini ya dhahabu kwenda nje ya nchi.

Kutokana na agizo hilo, Rais Magufuli aliagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuzuia makontena 262 yenye mchanga unaodaiwa kuwa na madini usisafirishwe kwenda nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Deusdedit Kakoko, alisema baada ya Rais kushuhudia makontena hayo, Alhamisi iliyopita walianzisha operesheni maalumu na kubaini makontena 262 yaliyokuwa na mchanga wa dhahabu tayari kwa kusafirishwa nje.

Alisema makontena hayo ni mali ya mgodi wa Buzwagi, unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia yaliyokuwa yamehifadhiwa bandari kavu ya Mofed iliyopo Kurasini, Temeke.


Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Acacia, Asa Mwaipopo, alisema makontena hayo ni ya mchanga wa madini ya shaba na yalifikishwa bandarini kabla ya zuio la Rais Magufuli.

No comments