SERIKALI YANUNUA MTAMBO WA KISASA WA MIL 101
Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele
(katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar
es Salaam kuhusu kuanza kazi kwa mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X
Ray Fluorescence (EDXRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara.Kutoka
kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Ubora wa Bidhaa, Bw. Daniel Ndiyo,
Mkurugenzi Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Nchini, Bw. Sabanitho
Mtega kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw. George
Kasinga pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za
Vinasaba,Bw. David Elias.
Baadhi ya
watumishi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Waandishi wa
Habari wakimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele (hayupo
pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kuhusu kuanza kazi kwa
mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X Ray Fluorescence (EDXRF) kwa ajili
ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara. Mtambo huo umefungwa kwenye Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoani Mbeya.
Mtambo wa Energy
Dispersive X – Ray Fluorescence (EDXRF) kushoto unaotumika kupima sampuli
mbalimbali zenye asili ya yabisi na vimiminika kama vile vyakula, bidhaa za
mafuta, maji, simenti, makaa ya mawe, bidhaa za chuma ili
kutambua kiwango cha madini kilichomo ndani ya sampuli hizo. Mtambo huo
umefungwa kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini, Mkoani Mbeya.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wakala
wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamenunua mtambo mpya wa kisasa
unaojulikana kama ‘Energy Dispersive X-Ray Fluorescence Spectrometer’ (EDXRF)
kwa ajili ya kurahisisha uchunguzi wa kimaabara.
Mtambo
huo uliogharimu kiasi cha shilingi 101,785,200 umesimikwa katika Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya kuanzia
Februari 21 hadi 23 mwaka huu.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali. Prof. Samwel
Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya mtambo
huo.
Prof.
Manyele amesema kuwa mtambo huo umesimikwa mkoani mbeya ikiwa ni moja ya hatua
za kuboresha maabara za Kanda zilizopo Arusha, Dodoma, Mbeya, Mtwara na Mwanza,
kusogeza shughuli za uchunguzi karibu na wananchi ili kupunguza gharama za
kusafirisha sampuli kuja mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.
“Kuwepo
kwa mtambo huo ni suluhisho kwa Serikali, Wizara, Viwanda, Mashirika,
Wachimbaji wa madini, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla ambao walikuwa
wanahitaji kufahamu ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali za viwandani na
mashambani, kutambua uwepo wa madini ya thamani kwenye udongo na bidhaa za vito
pamoja na sampuli zinazohusiana na usalama wa afya na mazingira,”alisema Prof.
Manyele.
Ameyataja
matumizi mengine ya mtambo huo kuwa ni kufanya uchunguzi wa sampuli za
migodini, kupima bidhaa za mbao ili kubaini kiwango cha kemikali zinazotumika
kutibu mbao, kupima sampuli za mafuta ya kula kwa kuangalia kiwango cha madini
ya phosphorus, kupima sampuli za pembejeo za kilimo pamoja na kufanya uchunguzi
wa sampuli na vielelezo vinavyohusiana na makosa ya jinai.
Prof.
Manyele amefafanua hoja zitakazojibiwa na matumizi ya mtambo huo zikiwemo za
kufahamu dhahabu kiasi gani ipo katika udongo unaohitaji kuchenjuliwa, kufahamu
mbogamboga zinazolimwa bondeni zina kiasi gani cha madini yanayoathiri
watumiaji, kufahamu kiasi cha uranium katika ardhi na vyanzo vya maji pamoja na
kufahamu athari za aina ya madini yaliyopo katika maji ya visima virefu na
vifupi kwa watumiaji.
Aidha,
Mkemia Mkuu amebainisha kuwa baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo, Maabara ya
Nyanda za juu kusini itakua na majukumu ya kukusanya sampuli za vinasaba vya
binadamu (DNA) pamoja na kuwa kituo rasmi cha kukusanyia sampuli nyingine
mbalimbali.
Maabara
hiyo kwa sasa ipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ambapo kuanzia mwezi
Aprili mwaka huu itahamia katika eneo la
Lwambi lililopo mkoani humo.
No comments