MWAKIFAMBA AKANUSHA UJUMBE ULIONEZWA MITANDAONI
Rais wa Shirikisho la
Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba amekana kuhusika na utumaji wa ujumbe katika
mitandao ya kijamii juu ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari.
Kauli hiyo imetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho hilo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari juu ya ujumbe huo uliokuwa ukisambazwa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii na kumuhusisha Rais wa Shirikisho hilo.
Mwakifamba amesema kuwa
ujumbe huo umeeleza kuwa Rais wa
shirikisho hilo atakuwa na mkutano na
waandishi wa habari utakaohusu wasanii waliokipigia kampeni Chama cha Mapinduzi
(CCM) na kutolipwa fedha zao pamoja na kuunga mkono jitihada za msanii Wema
Sepetu kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Kiukweli sikushiriki
kwa namna yoyote katika kuuandika ujumbe
huo na nimesikitishwa kuona kwamba huo ujumbe unasambazwa ukiwa na jina langu
hivyo umeniletea picha mbaya kwani ni kinyume na taratibu na sheria za
Shirikisho,”alisema Mwakifamba.
Amefafanua kuwa
Shirikisho hilo sio chama cha siasa na hawajasajiliwa na msajili wa vyama vya
siasa bali wamejisajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kazi zote
zinafanyika kwa Sheria Na. 4 ya mwaka 1976 ambayo iko chini ya Bodi ya Filamu
Tanzania.
Ameongeza kuwa
mwanachama wa shirikisho hilo hafungwi kuwa mwanachama wa chama chochote cha
siasa lakini kwa mujibu wa katiba ya vyama na shirikisho ni marufuku siasa
kuletwa katika shirikisho au vyama vyake.
Kwa upande wake Afisa
Mipango wa Chama cha Waigizaji, Saimon Mwapagaja ametoa rai kwa wananchi
wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa lengo la kuchafua majina ya watu
kuacha tabia hiyo kwani inashusha hadhi ya mtu husika na sio utaratibu mzuri.
“Changamoto tulizonazo
katika tasnia ya filamu ni nyingi sana hivyo ifike wakati wasanii tuanze
kuangalia vitu vya msingi na vyenye tija vitakavyomaliza changamoto hizo, pia
wananchi wapunguze kujiamulia kufanya mambo ambayo baadae yanaweza
kumsababishia muhusika matatizo mabukwa,” alisema Mwapagaja.
No comments