JITIHADA ZA KUBORESHA HUDUMA YA MACHO, SMZ YAKABIDHIWA VIFAA VYA MILIONI 78
Waziri
wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo (Kushoto), Mbunge wa Jimbo la Chwaka,
Bhagwanji Meisuria (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa SightSavers, Gosbert
Katunzi (kulia) wakifurahia jambo baada
kumalizika kwa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya huduma za macho
visiwani Zanzibar.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo
(katikati) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Chwaka, Bhagwanji Meisuria (kushoto)
wakikabidhiwa moja ya vifaa vya huduma za macho vilivyotolewa na Mkurugenzi wa
SightSavers, Gosbert Katunzi. Makabidhiano hayo yamefanyika hivi karibuni
visiwani Zanzibar.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo akitoa
neno la shukrani baada ya kukabidhiwa vifaa vya huduma ya macho kutoka shirika
la SightSavers, kutoka kulia ni Mkurugenzi wa shirika hilo, Gosbert
Katunzi pamoja na Mbunge wa
Jimbo la Chwaka, Bhagwanji Meisuria. Makabidhiano hayo yamefanyika hivi
karibuni visiwani Zanzibar.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Shirika la kimataifa
lisilo la kiserikali la Sightsavers limekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi 78,765,898 kwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ili visaidie katika kuboresha huduma za macho na
kutokomeza upofu unaoweza kutibika.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa
hivi karibuni Mjini Unguja na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Gosbert Katunzi
ambaye alisema msaada huo ni mwendelezo wa mkakati wa shirika hilo kusaidia
juhudi za Serikali katika kuinua huduma za Afya.
Katunzi alisema tangu
mwaka 2012-2016 jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetumika katika kutoa misaada
kwenye sekta ya afya ambapo vifaa pekee vimegharimu jumla ya kiasi cha shilingi
309,419,399.
Pia jumla ya shilingi
bilioni 1.3 zimetumika katika kukarabati majengo ya matibabu ya macho katika
Hospitali za Mnazi Mmoja, Wete na Chakechake Vision Centre, kusomesha wataalam
wa macho wa kada mbalimbali, manunuzi ya dawa, kufanya uhamasishaji jamii
pamoja na kuwezesha huduma karibu na wananchi.
“Katika kipindi cha
miaka mitano wananchi takribani 1,065,060 wamenufaika na huduma za uchunguzi wa
macho ambapo kati ya wananchi 4,307 waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho
watoto ni 408, waliopatiwa miwani ni 18,529 na waliopatiwa matibabu mengine ya
macho ni 300,640,” alisema Katunzi.
Aidha, Katunzi
alivitaja baadhi ya vifaa vilivyotolewa na taasisi yake kuwa ni kifaa cha
kuchunguza saratani ya macho pamoja na
vifaa vya uchunguzi wa macho(uoni) kiujumla pamoja na lensi mbalimbali
za kutengenezea miwani ya watoto na watu wazima.
Amefafanua kuwa
Sightsavers imekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za afya ya macho na kuendelea
kufanya maboresho zaidi katika vituo mbalimbali vya afya ili kutokomeza upofu
unaozuilika hivyo kuwa na Taifa lisilokuwa na magonjwa yanayozuilika.
Pia Katunzi alimshukuru
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo pamoja
na watendaji wa Wizara yake kwa kudumisha ushirikiano na taasisi yake pamoja na
wadau mbalimbali wa afya katika kuhakikisha wananchi wa visiwani wanafikiwa na
huduma za afya.
Shirika la Sightsavers
ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linalofanya kazi kwa ushirikiano
wa nchi zinazoendelea katika kuzuia upofu unaozuilika, pamoja na kusaidia
wagonjwa wa macho wenye uoni hafifu na ulemavu unaotokana na magonjwa ya macho,
Sightsavers ilianza kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu
mwaka 2006.
No comments