WATOTO KUPIMWA SARATANI BURE
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Asasi
ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania wameandaa huduma ya upimaji wa
saratani ya watoto bila malipo itakayotolewa Februari 18 mwaka huu katika
viwanja vya Donbosco vilivyopo Upanga, Jijini Dar es Salaam.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje – Marafiki wa
Watoto wenye Saratani Tanzania, Janeth Manoni alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu utoaji wa elimu juu ya kansa ya watoto.
Bi.
Janeth amesema kuwa saratani ya watoto ni janga kubwa ambalo wananchi wengi
hawalifahamu kama linaathiri kwa kiasi kikubwa hivyo lengo la Asasi hiyo ni
kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
”Utafiti
uliofanywa mwaka 2015/2016 umeonyesha kuwa Tanzania tunategemea kuwa na watu
40,000 ambao watakutwa na saratani kwa kila mwaka ambapo kati yao watoto ni
2500 hivyo, janga hili ni kubwa kwa watoto na linahitaji kupewa kipaumbele ili
kupunguza idadi yake”,alisema Bi. Janeth.
Ameongeza
kuwa saratani za watoto zikigundulika mapema zina uwezo wa kupona kwa asilimia
80 lakini tatizo lilopo ni kucheleweshwa kufikishwa hospitali kwa sababu wazazi
wengi hawafahamu dalili za awali za kansa hiyo.
Kwa
upande wake Muasisi wa Asasi ya Saratani Tanzania Franklin Mtei, amesema kuwa
wanaharakati wa sekta ya afya wamejitolea kutoa elimu juu ya dalili za saratani
ya watoto kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kutoa elimu siku hiyo ya
upimaji.
Ametoa
wito kwa wananchi kujitokeza siku hiyo na kujijengea utamaduni wa kupima afya
mara kwa mara pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka kupata magonjwa mengine
yasiyoambukiza.
No comments