Breaking News

VIJANA WASHAULIWA KUTUMIA FUSRA ZILIZOPO SEKTA YA KILIMO

 Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Umoja wa Kilimo cha mbogamboga, matunda na nafaka umetoa wito kwa vijana kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Kilimo na si kusubiri kuajiriwa.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Umoja huo Joseph Kunguru wakati akizungumza na waandhishi wa habari kuhusu mradi kambi ya kilimo ulioanzishwa na Umoja huo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa wameandaa mradi huo kwa lengo la kuhamasisha vijana kuona kilimo ni ajira na pia kilimo ni biashara.
 
 “Tuna wanachama 74 ambao wanatarajia kwenda kambini ambapo kati ya hao vijana 23 ni wahitimu wa vyuo vikuu, watapatiwa mashamba, mbegu, vitendea kazi pamoja na chakula katika muda watakao kuwa huko ili kuwafanya waweze kumudu katika shughuli za kilimo” alisema Bwa. Kunguru.

Aidha, alisema kuwa umoja huo unaunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na madawa ya kulevya kwa kuwachukua vijana ambao wameshapata matibabu kujiunga na mradi huo ili kuweza kuwafanya wasirudi tena vijiweni.

Akifafanua zaidi Bwa. Kunguru alisema kuwa ili kuendesha umoja huo kiuchumi kila mwanachama kwenye kila zao atachangia asilimia tano ya mapato kwenye umoja kama fidia ya vifaa pamoja na mbegu walizopata kutoka kwenye umoja huo.

Mbali na hayo, umoja huo umepanga kuanzisha ligi ya mpira wa miguu itakayojulikana kama Kilimo Kapu kwa lengo la kuhamasisha vijana kujiunga kwa pamoja kama vikundi ili kuweza kuwa na kambi za maendeleo ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuinua pato la taifa.

No comments