TGGA KUADHIMISHA ‘THINKING DAY’ KWA KUFANYA SHUGHULI ZA KIJAMII.
Kamishna
wa Makao Makuu wa Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Rosaldina Majuva
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya chama hicho
wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam,
kutoka kulia Kamishna Mkuu wa chama hicho Symphorosa Hangi na Katibu wa chama
hicho, Grace Shaba.
Katibu wa chama cha Tanzania Girl Guides Association (TGGA),
Grace Shaba akifafanua kuhusu malengo ya chama hicho wakati wa mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna Mkuu wa chama hicho Symphorosa Hangi,
kushoto ni Kamishna wa Makao Makuu wa chama
hicho, Rosaldina Majuva.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Tanzania
Girl Guides Association (TGGA) wanategemea kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa
chama hicho kwa njia ya kufanya shughuli mbalimbali za kuisaidia jamii.
Maadhimisho
hayo yanayojulikana kama ‘thinking day’ yatafanyika Februari 22 mwaka huu
ambapo shughuli za kuisaidia jamii zitaanza Februari 10 mwaka huu.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Makao Makuu wa Chama hicho,
Rosaldina Majuva alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maadhimisho hayo.
Bi.
Rosaldina amesema kuwa siku ya maadhimisho ya chama hicho inaambatana na siku
ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa waasisi wao akiwemo Lord Baden Powell ambaye
alikuwa kiongozi wa Boy Scout pamoja na Kamishna Mkuu wa Girl Guides na Girl
Scouts, Lady Olave Baden Powell (mkewe).
“Tumepanga
kuadhimisha siku hii muhimu kwa kufanya shughuli za kijamii zikiwemo za kutoa
misaada kwa wahitaji, kutunza mazingira kwa kufanya usafi katika eneo la Coco
Beach na Magomeni na kupanda miti, kutoa elimu ya kujithamini, kujitambua na
kukataza unyanyasaji pamoja na kutembelea kituo cha wazee wa Kigamboni,”alisema
Bi. Rosaldina.
Kwa
upande wake Katibu wa chama hicho, Grace Shaba amefafanua kuwa chama hicho kimelenga
kupanua uelewa wa wanawake kwa ujumla kuhusu uzalendo, majukumu ya nchi yao,
kujenga ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia kambi za mafunzo,
kutembelea na kuwasiliana kwa njia za teknohama pamoja na kuwa tayari kufanya
kazi kwa manufaa yao na ya Taifa.
“Dira
yetu ni kuwa na jamii yenye wasichana na wanawake waliowezeshwa kufikia uwezo
wa juu kabisa katika kutimiza malengo yao na kuwa rasilimali bora ya
Taifa,”alisema Bi. Grace.
Nae
Kamishna Mkuu wa Tanzania Girl Guides Association, Symphorosa Hangi amesisitiza
wanawake na watoto wa kike kujiunga na chama hicho kwani kinatoa elimu ya
masuala ya kijamii na kiuchumi yatakayosaidia kuwainua wanawake na watoto
pamoja na taifa kwa ujumla.
Mpaka
sasa kwa Tanzania,chama hicho kipo katika mikoa 22 kikiwa na jumla ya wanachama
101,824.
No comments