SAKATA LA WATANZANIA 180 WAFUKUZWA MSUMBIJI BADO UTATA KIINI CHA CHANZO
Idadi
ya Watanzania wanaorudishwa kutoka nchi ya Msumbiji walikokuwa wakiishi,
imezidi kuongezeka na kufikia 180 huku kukiwa na madai ya kuwafanyia vitendo
vya kikatili.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Ofisa Uhamiaji mkoani Mtwara, Rose Mhagama alisema
taarifa ambazo wamezipata hadi sasa ni kwamba bado Watanzania wengi wamefungiwa
katika mahabusu za nchini humo na wanarudishwa kwa makundi.
Mhagama
alisema sababu za kurudishwa kwa Watanzania hao bado hazijafahamika ila
uchunguzi wa kina unaonyesha kwamba katika maeneo ya Mtepweshi na Nanyupu
nchini humo, kuna migodi ya madini inayomilikiwa na raia kutoka moja ya nchi za
Magharibi, anayedaiwa kufadhili askari wa nchi hiyo kuwafukuza Watanzania.
“Sijui
ni kwanini na sifikirii sana kwamba Watanzania pekee ndio wapo kwenye maeneo
hayo, kimsingi taarifa ambazo tunazo ni kwamba anaona kama Watanzania ndio
wanakwenda kupora zile mali zilizopo katika machimbo hayo.
“Kiukweli
zoezi hili linaleta sintofahamu nyingi kwa sababu unajiuliza kama kweli ni
zoezi rasmi, kwanini wanawachania hati zao za kusafiria na kuwanyang’anya vitu
vyao, inaonyesha wana nia ya kuwapora Watanzania mali zao au kutowatendea
haki,” alisema.
Wakati
ofisa hiyo akisema idadi ya Watanzania waliofukuzwa Msumbiji ni 180, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba amesema idadi ni watu 132 na
ikitarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na operesheni ya kuwarudisha nyumbani
wahamiaji haramu.
Alisema
Februari 11, Watanzania 58 walirudishwa nchini kutoka Msumbiji, Februari 14
walirudishwa Watanzania 24 na jana walirudishwa wengine 50 ikiwa ni mwendelezo
wa operesheni hiyo inayoendelea nchini humo.
Akizungumzia
suala hilo jana jijini Dar es Salaam, Dk Kolimba alisema operesheni hiyo
haijawalenga Watanzania pekee bali pia raia wa nchi nyingine walioingia
Msumbiji kinyume cha taratibu.
Dk
Kolimba alisema operesheni hiyo inaendeshwa katika mji wa Monte Puez uliopo
Jimbo la Cabo Delgado na mji huo una Watanzania 3,000 wanaoishi huko na kwamba
idadi ya watakaoondolewa huko inaweza kuongezeka zaidi.
“Tunaendelea
kufuatilia tuhuma za baadhi ya Watanzania kwamba walifanyiwa ukatili wakati
wanarudishwa nyumbani ili tujue hatua za kuchukua. Ubalozi wetu unashirikiana
na serikali ya Msumbiji katika kuhakikisha Watanzania hawapati matatizo katika
operesheni hiyo,” alisema Dk Kolimba.
Dk
Kolimba alisema Serikali inaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na
serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao. Hata
hivyo, alisisitiza kwamba uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni mzuri.
No comments