MKEMIA MKUU KUENDELEA KUTOA MAFUNZO KWA WADAU WAKE KWA LENGO LA KUWAJENGEA UWEZO
Mkemia
Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele (katikati) akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) leo
Jijini Dar es Salaam kuhusu mafunzo ya
wasafirishaji na watumiaji wa Kemikali nchini, kutoka kulia ni Kaimu Meneja wa
Maabara ya Kanda ya Mashariki, Everlight Matinga na Mkurugenzi wa Idara ya
Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali nchini,Sabanitho Mtega, (kutoka kushoto),
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, David Elias
pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Biashara,George Kasinga
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa Mkemia
Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele uliohusu mafunzo ya wasafirishaji na watumiaji wa
kemikali nchini, leo Jijini Dar es
Salaam.
Wakala wa Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) wamejipanga kuendelea kuendesha mafunzo kwa
wadau wa Kanda ya Mashariki wanaohusika na kemikali ili kuhakikisha kemikali zinatumika
vema na kwa njia salama.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wasafirishaji na watumiaji wa
kemikali nchini.
Prof. Manyele amesema
kuwa wakala hufanya usajili na ukaguzi kwa wadau wote wanaohusika na kemikali
wakiwemo waagizaji, watengenezaji, wasafirishaji, watumiaji, wanaosafirisha nje
ya nchi au yeyote yule anayehusika na kemikali kwa njia moja au nyingine.
Pia ukaguzi huo
unahusisha mahali ambapo kemikali zinatumika, zinatunzwa au kuhifadhiwa.
“Kuanzia mwaka 2012
hadi sasa, wadau wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliopatiwa mafunzo ni 642
wakiwemo Askari wa Jeshi la Polisi Usalama Barabarani Tanzania Bara, wasimamizi wa shughuli za uzalishaji
kwenye viwanda, wasambazaji, wasafirishaji wa kemikali pamoja na madereva
wanaosafirisha kemikali., hivyo baada ya kuona umuhimu wake tumeamua kuendelea
na mafunzo haya kwa wadau wetu wengine,” alisema Prof.Manyele.
Prof. Manyele
ameongeza kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa siku mbili kwa kila kundi katika
makundi matatu yakiwemo ya wasimamizi wa shughuli zinazohusisha kemikali
watakaoanza tarehe 21- 22/02/2017, Mawakala wa Forodha watakaoanza tarehe
23-24/02/2017 pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali kuanzia tarehe
10-11/03/2017.
Aidha, Wakala Mkuu wa
Serikali amefafanua kuwa Wakala hautaruhusu mdau ambaye hajapitia mafunzo hayo
kuhusika katika shughuli yoyote ya kemikali kwa kutumia, kuhifadhi,
kusafirisha, kutoa bandarini na hata kuagiza kutoka nje ya nchi hivyo
akasisistiza umuhimu wa wahusika kuhudhuria mafunzo hayo.
Ametoa rai kwa wadau
hao kuwahi kuhudhuria mafunzo haya ili kutekeleza matakwa ya Sheria Na. 3 ya
mwaka 2003 ya Udhibiti na Usimamizi wa kemikali pamoja na kuepuka usumbufu
utakaoweza kujitokeza kwa sababu ya kukosa mafunzo.
No comments