MTUMISHI WA UMMA ATAKAYESHINDWA KUWASILISHA CHETI AU INDEX NUMBER, AMEJIONDOA KAZINI MWENYEWE
MTUMISHI wa umma atakayeshindwa kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), itakapofika Machi mosi mwaka huu, atakuwa kajiondoa kazini mwenyewe, imeelezwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora), Angellah Kairuki alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati
akifungua Mkutano wa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki.
“Watendaji wakuu ninawaomba msimamie uhakiki wa vyeti ili
watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki,” alisisitiza Kairuki, katika
taarifa iliyotolewa na wizara yake.
Aliongeza kwamba serikali ilisitisha ajira mpya ili kupisha kazi
ya kuondoa watumishi hewa, ambayo imefika ukingoni na siku za karibuni, ajira
zitarudishwa.
Akiwa mjini Dodoma, Septemba mwaka jana, wakati wa kuapishwa kwa
wakurugenzi watendaji wapya 13 walioteuliwa Septemba 10, mwaka huu, Kairuki
alisema kuanzia serikali imewaondoa watumishi hewa 17,201 kwenye utumishi wa
umma na kazi hiyo inaendelea.
Kairuki aliwataka watendaji wakuu kuweka mikakati ya kuepuka
watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwa sababu jambo hilo, limeumiza na
kupoteza rasilimalifedha nyingi za serikali.
Alisema anatambua kuna wakala zenye upungufu wa watumishi, hivyo
zinaingia gharama kubwa za kuajiri wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo
alielekeza kila Mtendaji Mkuu ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji
halisi ya watumishi.
Pamoja na hilo, Kairuki alielekeza wakala zenye watumishi wa
mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama kweli watumishi hao wanahitajika kwa
kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya taasisi.
Aliongeza kuwa yapo malalamiko kuhusu suala la maadili na
uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali.
Aliainisha masuala hayo ni pamoja na watumishi hewa, taarifa chafu
za watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, kutosimamia
ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza
majukumu ya msingi ya wakala.
Alifafanua kuwa amegundua kupitia taarifa mbalimbali kuwepo kwa
changamoto ya mawasiliano hafifu kati ya wizara mama na wakala zilizo chini yao
ambapo taarifa kutoka katika wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata
zinapochambuliwa na wizara mama, hazitoa mrejesho kwenda katika wakala.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi), Dk Laurean Ndumbaro alizitaka
wakala za serikali kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha
utendaji kazi na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.
Chanzo-Habarileo
No comments