KUTOKA MBEYA: MWENYEKITI WA CCM APIGWA RISASI BAADA YA KUVAMIWA
Mwenyekiti was CCM wilaya ya Mbeya mjini ndugu Ephrahim Mwaitenda akifikishwa hospitali ya Rufaa mkoa wa Mbeya asubuhi ya leo Jumatatu Januari 30,2017,Kulia ni kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya ndugu Lobe Zongo akimpokea Mwaitenda katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya baada ya kudaiwa kupigwa risasi.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Mbeya mjini,
Ephreim Mwaitenda amenusurika kifo baada ya watu wasiofahamika
kumvamia shambani kwake wilayani Kyela akiwa amelala usiku na kumjeruhi
kwa risasi mgongoni.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoani Mbeya Emmanuel Lukula amesema Mwaitenda alipigwa risasi baada ya
watu hao kuvunja dirisha usiku na kuchana nyavu za dirisha kisha
kupenyeza mtutu na kumpata Mwaitenda mgongoni
Lukula alisema baada ya kufyatua risasi watu hao walitokomea
kusikojulikana ambapo Mwaitenda alidhani kuwa ni simu imepasuka
lakini alitahamaki akivuja damu mgongoni.
Kaimu Kamanda Likula alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa
nane usiku ambapo Mwenyekiti alitoa taarifa kituo cha Polisi Kyela.
Alisema askari walifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi hadi
hospitali ya Wilaya ya Kyela na kufanikiwa kuondoa baadhi ya
risasi zilizotengenezwa kwa goroli na ambazo zimetumiwa na
bunduki iliyotengenezwa kienyeji.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo
alisema majeruhi amefikishwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa ajili ya
matibabu zaidi.
Aidha Katibu Zongo amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufika haraka
eneo la tukio pamoja na Madaktari ambao wanafanya juhudi za kuondoa
risasi zilizokwama mgongoni.
Kaimu Kamanda Lukula alisema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na
tukio hilo na uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watu waliofanya uhalifu
huo walidondosha baadhi ya vitu ambapo wanavifanyia kazi.
Aidha baadhi ya wananchi Mkoa wa Mbeya na Wanasiasa
wanalihusisha tukio hilo na siasa kutokana na mwaka huu ni Uchaguzi wa
Vyama vya siasa.
“Lazima waliofanya hivyo ni wagombea wa nafasi Fulani ndani ya
Chama na walitaka kummalizi ili waweze kupita kirahisi lakini
tusubiri ripoti ya Jeshi la Polisi tuone wahusika wenyewe” alisema mmoja
wawananchi wa sharti la kuhifadhi jina lake.
Chanzo- Mbeya yetu blog
No comments