MHE LOWASA ATOA NENO JUU YA MSTAKABALI WA AMANI NA MSHIKAMANO ULIOPO NCHINI
CHAMA
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewaomba viongozi wakuu wastaafu
nchini, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuchukua hatua za kuondoa tofauti
zinazoanza kujitokeza nchini ikiwemo uendeshaji wa siasa za chuki zinazofanyika
mbele ya macho yao.
Ombi
hilo limetolewa jana na waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu
ya CHADEMA Taifa, Edward Lowassa alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa
kata ya Isagenhe wilayani Kahama mkoani Shinyanga katika mkutano wa kampeni za
kumnadi mgombea udiwani wa CHADEMA katika kata hiyo Richard Luziga.
Lowassa
alisema hivi sasa kuna mambo mabaya ya chuki yanafanyika huku waliokuwa
viongozi wakuu katika nchi hii wakishuhudia kwa macho bila kuchukua hatua ya
kukemea hali inayoweza kusababisha kutoweka kwa hali ya amani na utulivu
iliyopo hivi sasa hapa nchini.
Alisema
kwa kadri siku zinavyokwenda baadhi ya watu wameanza kuendesha siasa za chuki
huku wengine wakimtabiria yeye (Lowassa) kifo na kwamba siasa hizo haziwezi
kuwasaidia lolote watanzania na hivyo kuna kila sababu kwa viongozi wastaafu
kukaa na kuangalia jinsi gani watanzania wataachana na siasa hizo.
“Ninawaomba
mzee Mkapa na mzee Mwinyi njooni msawazishe mambo haya, ondoeni mambo ya chuki
yanayoanza kufanyika hivi sasa hapa nchini, watusaidie kuondoa tofauti hizi,
watu wapingane kwa hoja bila ya kupigana na tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa
na utulivu na hatutokuwa na mambo mengine makubwa mabaya,”
“Hizi
chuki ni mbaya sana wanazielekeza kwa watu na kuzifanya ziwe mbaya zaidi, kwa
mfano wapo walionitabiria kifo, lakini mwenyezi mungu amewatanguliza mbele ya
haki kabla yangu, nasema siasa za chuki hazitusaidii lolote katika nchi hii ni
vizuri tujenge umoja na mshikamano katika nchi yetu,” alieleza Lowassa.
Kwa
upande mwingine Lowassa alimuombea kura mgombea udiwani katika uchaguzi mdogo
unaofanyika katika kata 20 nchini ikiwemo kata hiyo ya Isagenhe, Richard na
kwamba iwapo watamchagua watakuwa wamepata mwakilishi mwenye uwezo wa
kuwawakilisha vyema katika baraza la madiwani na kuwaondolea kero zinazowakabili.
Akizungumza
katika mkutano huo kada mwingine wa CHADEMA, Khamis Mgeja aliyewahi kuwa
mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, aliwataka wakazi wa kata ya Isagenhe
kupuuza ‘porojo’ zinazoelezwa mara kwa mara na viongozi wa CCM wakidai watu
wote waliohama CCM na kujiunga na CHADEMA ni mafisadi na wezi.
Mgeja
huku akishangiliwa alisema madai hayo siyo ya kweli kwa vile mafisadi na wezi
wengi wamo ndani ya CCM ambapo alidai iwapo kweli wezi anatoa ruhusa kwa askari
polisi wawakamate wakati wowote na kuwafikisha mahakamani ili wajibu mashitaka
watakayofunguliwa.
“Ndugu
zangu tupo hapa kumnadi mgombea wetu wa CHADEMA, ndugu yetu Richard Luziga,
huyu ndiye anayefaa kuwa diwani wenu, ni mchapa kazi, lakini pia nitumie nafasi
hii kuwaomba msikubali kuendelea kudanganywa na wenzetu hawa wa CCM, kila siku
wanapiga kelele kudai eti sisi tuliohama CCM tulikuwa mafisadi na wezi, siyo
kweli,”
“Sisi
siyo wajinga kuondoka ndani CCM, na niwaeleze wazi mikia yetu ni migumu kweli
haitatokea ikatike ngoo’ wala siyo wezi au mafisadi kama inavyodaiwa, ukiwa
mwizi au fisadi huwezi kuhama CCM, maana hii CCM ya sasa siyo ile ya mwalimu
(Nyerere) hii imemaliza pumzi, mnasubiri nini kuihama?” alihoji Mgeja.
Nao
makada wengine wa CHADEMA, James Lembeli na John Guninita waliwataka wakazi wa
kata ya Isagenhe wakubali kufanya mabadiliko kama inavyotokea katika nchi
nyingine ulimwenguni ikiwemo Marekani ambayo wananchi wake wameamua kumchagua
mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump na kumpiga chini mgombea Hilary
Clinton wa Democratic.
Kwa
upande wake mgombea udiwani katika kata hiyo, Richard Luziga aliwaomba wananchi
wamchague kwa kura nyingi na kwamba iwapo atashinda mambo atakayoyapa
kipaumbele katika kuyashughulikia ni ujenzi wa zahanati, umeme na kufikisha
maji katika kata hiyo.
No comments