MAJAMBAZI YAPORA MAMILIONI YA FEDHA JIJINI DAR MBELE YA ASKARI POLISI
Mfanyakazi
wa kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share mwenye asili ya China, Cheng Deng
akionesha maofisa wa polisi dirisha la gari lililovunjwa kioo na majambazi na
kupora Sh milioni 25. (Picha na Fadhili Akida).
WATU
wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya
shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la
Tazara, Dar es Salaam.
Gazeti
hili lilishuhudia tukio hilo jana, saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye
foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara.
Watu
hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata
pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.
Aidha
taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke,
Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo wa
usalama barabarani.
Wakati
tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari doria
zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa Barabara ya
Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu hao waliokuwa
wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na Jeshi la Polisi.
Majambazi
hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4
yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun
Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard
Charles.
Kwenye
gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China,
aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.
Kwa
mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki
eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki
aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita
kutoka barabara ya Mandela.
Charles
alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha
lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla
ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.
“Kwa
kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili mmoja
upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola nifungue mlango
niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo cha nyuma kwa kutumia
kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na kutokomea” alisema Richard.
Askari
wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio hilo
wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina
lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha
pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo linalohatarisha usalama wao na mali zao.
“Kama
walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini wasingeomba hata
‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni tatizo, hasa katika
kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu wanatakiwa kuchukua
tahadhari mapema.” alisema askari huyo.
Hata
hivyo mwandishi wa habari alipokwenda katika ofisi za kampuni hiyo kujua kwa
undani tukio hilo lilivyotokea, alimkuta mlinzi ambaye alikiri kutokea kwa
tukio hilo.
Hata
hivyo mlinzi huyo alimwelekeza mwandishi kuongea na mmoja wa wahusika wa
kampuni hiyo mwenye asili ya China ambaye baada ya mwandishi kujitambulisha,
alikataa kutokea kwa wizi huo.
Pamoja
na kukataa alimwamuru mwandishi aondoke katika ofisi zao huku akisisitiza
hakuna tukio hilo na hakutaka kuzungumza zaidi.
Hata
hivyo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Simon Sirro
alipopigiwa simu na gazeti hili jana ili kupata ufafanuzi zaidi wa tukio hilo
simu yake iliita bila majibu na baadae alipokea na kusema yupo kwenye kikao.
Mwandishi
alimtumia ujumbe mfupi wa simu kueleza tukio hilo akimuuliza kama ana taarifa
lakini hakujibu ujumbe huo na alipopigiwa tena baadae jana, simu iliita bila
majibu.
Chanzo-Habarileo
Hivi kila siku matukio haya yanaripotiwa na msisitizo wa polisi ni kuomba ulinzi wa polisi kama unasafirisha kiasi kikubwa cha pesa. Unafikiri kwanini watu hawaombi ulinzi wa polisi?
ReplyDelete