Breaking News

RAIS WA GAMBIA AGOMA KUACHIA MADARAKA ATANGAZA HALI YA HATARI NCHINI HUMO

Bunge la Gambia limerefusha utawala wa Rais Yahya Jammeh kwa miezi mitatu baada ya kiongozi huyo kutangaza hali ya hatari katika taifa hilo na ikiwa imebaki siku moja tu kabla ya muhula wake kumalizika rasmi .

Tangazo la bunge kurefusha madaraka ya rais Jammeh kwa miezi mitatu yanafuatia amri iliyotangazwa na kiongozi huyo kutokana na kile alichokiita ni kuingiliwa kwa kiasi kikubwa na mataifa ya kigeni katika uchaguzi wa Desemba mosi na mambo ya ndani ya Gambia.

Kwa tangazo hilo wananchi wa Gambia "wamepigigwa marufuku kufanya matendo yoyote ya kutoheshimu sheria, kuchochea ghasia na kuvuruga amani".

Hali ya hatari
Kupitia Televisheni ya taifa, Rais Jammeh amesema kuwa, "Mimi Sheikh Profesa Alhaji Dr Yahya A.J.J. Jammeh rais wa Jamhuri ya kiislamu ya Gambia na Amiri Jeshi mkuu, natangaza hali ya hatari kwa nchi nzima ya Gambia kama hali ilivyo na ikiwa itaendelea inaweza kusababisha hali ya hatari kwa umma", amesema Jammeh.

Chini ya katiba ya Gambia hali hiyo ya hatari itadumu kwa kipindi cha siku 90 ambapo bunge la nchi hiyo tayari limepitisha azimio la kuithibitisha na hiyo inamaanisha rais Jammeh atasalia madarakani kwa kipindi cha miezi mitatu.

Marekani imemtaka rais Jammeh ambaye ameitawala Gambia kwa miaka 22 kuachia madaraka na kumkabidhi rais mteule Adama Barrow ambaye yupo nchini Senegal anakopanga kubakia hadi hapo kesho siku ya kuapishwa kwake.

Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa 15 ya magharibi mwa Afrika ECOWAS nayo imetoa wito kwa kiongozi huyo kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kuondoka mamlakani, wito unaoungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Umoja wa Afrika na wengine.

Jammeh amekataa ujumbe wa viongozi wawili wa ngazi ya juu wa Afrika Magharibi ambao walimtolea wito wa kuondoka.

Raia wa nje waondolewa
Kutokana na tangazo hilo, mataifa ya kigeni yamesema yatawaondoa raia wake, wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza imeandika katika tovuti yake kuwa "uwezekano wa kuingilia kijeshi na usumbufu wa kiraia ni mkubwa", tahadhari ambayo imeungwa mkono na Uholanzi kupitia mitandao ya kijamii ikiwataka raia wake kuepuka kusafiri labda ikiwa ni kwa umuhimu.

Wakala wa utalii wa Uingereza Thomas Cook kupitia taarifa yake imesema inapanga kuwaondoa wateja wake watalii wapatao 3500 kupitia uwanja wa ndege wa Banjul katika masaa 48 yajayo.

Tayari mawaziri wanne katika serikali ya rais Jammeh wamejiuzulu wiki hii ambao ni waziri wa fedha, waziri wa biashara, waziri wa utalii, na waziri wa mambo ya nje, na kuungana na waziri wa mawasiliano ambaye aliachia wadhifa wake wiki iliyopita na sasa yuko Senegal.

Raia nchini humo wameendelea kukimbia kutoka Gambia wakielekea nchi jirani za Senegal, Guinea-Bissau na Guinea.

Taarifa kutoka Nigeria zinasema maandalizi ya kuwapeleka wanajeshi kadhaa mjini Dakar Senegal yamekamilika hali inayohusishwa na kile kinachojiri nchini Gambia.

No comments