KUTOKA SHINYANGA: JAMBAZI SUGU AUAWA AKIJARIBU KUTOROKA POLISI SHINYANGA
Mwanamme mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu aliyejulikana kwa jina la Amos James Haruna mkazi wa mtaa wa Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa jeshi la polisi , wakati akijaribu kutoroka huku wengine nane wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kutumia silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Desemba 3,2016, kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema kulingana na kumbukumbu za wahalifu za polisi ndipo walibaini mtu huyo alikuwa ni jambazi sugu kutokana na kufanya uhalifu katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Amesema jambazi huyo alikutwa na silaha aina ya SMG yenye namba K5380 ikiwa na risasi 30 na zingine nane zikiwa kwenye mfuko akiwa kwenye gari yake yenye namba za usajili T 794 BZP Toyota Cresta alipohojiwa alikiri kufanya uhalifu mikoa ya Mwanza,Geita na Shinyanga.
“Polisi baada ya kumuhoji jambazi huyo sugu Novemba 30 mwaka huu aliwaeleza kuwa anayo bunduki nyingine aina ya SMG ambayo alidai huwa anaificha kwa mganga wa kienyeji e kijiji cha Busoka halmashauri ya mji wa Kahama aliondoka na polisi na alipokaribia eneo hilo kwenye mkusanyiko wa watu aliwaeleza wasimame na kushuka ndipo alipojaribu kutoroka na kupigwa risasi”anaeleza kamanda Muliro.
Kamanda Muliro alisema katika tukio hilo watuhumiwa wengine nane wamekamatwa wakiwemo wanawake wanne na wanaume wanne.
Na Stella Ibengwe-Malunde1 blog
No comments