BODI YA MIKOPO: WADAIWA SUGU WA KUANIKWA KATIKA VYA HABARI, UHAKIKI KUFANYIKA OFISI KWA OFISI KUANZIA 1 JAN 2017
BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni mwa
Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu kwenye
vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kuanzia
wale wa miaka 10 iliyopita.
Bodi
hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka huu, kwa
wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo, vinginevyo hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika kulipia gharama za
kuwasaka na kuendesha kesi.
Pamoja
na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa
marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri
wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki waajiriwa
wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB, na adhabu yao
itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo,
Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30 walioutoa,
wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha wenyewe kwa hiari, kulipa
madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.
“Tumeamua
kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa hawa wa
bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili waturejeshee fedha
zetu,” alisema Badru.
Aidha,
alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia na
kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa fursa ya
kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado haitoshelezi.
Alisema
bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye kuwaongezea
tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu, hivyo kinachofuata ni
utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa hiyo ya kujisalimisha.
Mkurugenzi
huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha majina na
picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa kulipa madeni yao,
watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usumbufu
wa kuwatafuta.
Alisema
utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi, kupata fursa
ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema wanafunzi wote
wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda muafaka uliowekwa
kisheria.
Badru
alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo,
imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo kutoka
miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na kutafuta ajira.
Aidha,
alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa waajiriwa
walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya mishahara yao hadi
asilimia 15.
“Tunawashukuru
sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii katika
eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi asilimia 30 na
zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo wa wabunge
walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.
Alisema
ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo
aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo imeanza
mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kupitia marekebisho
hayo ya sheria.
“Tumeunda
kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali nyeti,
kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya kuhakiki kila ofisi
ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha majina ya wanufaika wa
mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha michango hiyo kwa bodi,” alisema.
Alisema
waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia bodi
kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao, wataadhibiwa kwa
mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato hayo waliyoshindwa
kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha muda
wa miezi 36 jela.
“Lakini
pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka wenyewe
taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato, yeyote
atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.
Halikadhalika,
Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa mikopo hiyo
ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira, ambao nao wanatakiwa
kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila mwezi.
Akizungumzia
mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa wenyewe
madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha, yameongezeka kutoka Sh
bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni nane.
Alisema
tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe kwa hiari
na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na wengine wakiyapunguza.
Hadi
sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva, inazozidai kwa
wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140 pekee ndio zimelipwa.
Kwa
mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179 wamenufaika
na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu ianzishwe Juni, mwaka
1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa wanafunzi hao.
Jumla
ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya HESLB,
wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh trilioni 1.4, baada
ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria kuisha.
No comments