RAIS MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA MAKAMU WA RAIS WA CUBA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 03 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha na kuongeza uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwa manufaa ya wananchi wake.
Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema anatambua uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Cuba na kwamba Serikali yake imejipanga kuhakikisha uhusiano huu unaelekezwa katika maeneo yenye manufaa ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Rais Magufuli amemuomba Makamu huyo wa Rais wa Cuba kuwashawishi wawekezaji wa kutoka nchini mwake kuja hapa nchini kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu ili kurahisisha upatikanaji wa dawa na kupunguza gharama.
Pia, Rais Magufuli amemuomba Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa kuwashawishi wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na amewahakikishia kuwa wakiwa tayari Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kuendesha uzalishaji huo.
"Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa najua kuwa nchi yenu ina utaalamu wa kutosha katika uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa dawa za binadamu na masuala mengine mengi yanayohusu matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji, nakuomba uwaambie wafanyabiashara wa Cuba kuwa tunawakaribisha waje Tanzania kuwekeza na Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha" amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Cuba Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yake katika kuinua uchumi wa Tanzania na amemhakikishia kuwa Cuba ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kutumia utaalamu na uzoefu wake.
Amesema kwa kuanzia Cuba italeta wataalamu kwa ajili ya kuangalia namna itakavyotekeleza ombi la kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu na pia atazungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Cuba na kuwashawishi kuja hapa nchini kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.
"Mhe. Rais Magufuli natambua kuwa uhusiano wetu na Tanzania na Afrika ni wa kihistoria, sisi Cuba tumepiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi na teknolojia, nimekuja kukuhakikishia kuwa tutauendeleza uhusiano huu ili ulete manufaa kwenu na kwa wananchi wa Cuba" amesema Mhe. Mesa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Oktoba, 2016
No comments