VYUO VIKUU VYATAKIWA KUUNGA MKONO SERIKALI KATIKA KUJENGA TANZANIA YA VIWANDA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amevitaka vyuo vikuu
Tanzania kuunga mkono serikali ya Awamu ya Tano juu ya uanzishwaji wa viwanda
kuelekea uchumi wa kati.
Prof. Ndalichako
ameyasema hayo leo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam alipokuwa
akifungua maonyesho ya kumi na moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yatakayofanyika kwa siku tatu kuanzia leo Julai 20 mpaka Julai 22 mwaka huu.
“Vyuo vikuu
vinatakiwa kuangalia sera za nchi na mwelekeo wa Taifa kuelekea kukuza uchumi
wa viwanda kwa kuhakikisha wanatoa wataalamu ambao watashiriki katika uchumi wa
viwanda ambavyo vitaanzishwa nchini,” alifafanua Prof. Ndalichako.
Prof. Ndalichako
aliendelea kwa kusema kuwa Serikali iko katika mkakati wa kuboresha vyuo vya
ufundi kwa kuanzia na vyuo vitatu vya ufundi vya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya
ili kuboresha mafunzo wanayoyatoa kuendana na uhitaji uliopo katika uanzishwaji
wa viwanda.
Mbali na hayo,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inashirikiana na
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika uanzishwaji wa mafunzo katika
sekta adimu ikiwemo gesi kwa ajili ya kupata wataalamu watakaoajiriwa katika
viwanda vitakavyo anzishwa.
Vile vile wanafunzi
wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu hupewa maelekezo ya namna ya kuomba vyuo
kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE) katika maonyesho hayo.
Maonyesho ya Elimu
ya Juu, Sayansi na Teknolojia hufanyika kila mwaka yakiwa na Lengo la kutoa
elimu kwa wazazi na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu hapa nchi
waweze kujua kozi zinazotolewa katika vyuo hivyo pamoja na maelezo ya kozi
hizo.