Breaking News

TAEC HAKUNA MADHARA YA MIONZI KWA WANAOISHI KARIBU YA MINARA, WAFUNGUKA MIAKA MITATU YA RAIS DKT. SAMIA

Imeelezwa kuwa Ujenzi wa minara ya simu karibu na makazi ya watu hakuna madhara ya mionzi kwa wananchi wanaoishi katika maeneno ya jirani kama ambavyo jamii imekuwa na hofu kutokana na kupata taarifa zisizo sahihi.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala wakati akijibu swali katika kikao kazi na Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali kikao kinachoratibiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho amesema tume hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha Uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo wamepata mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kufanya kaguzi nyingi na kuwa na ofisi 63 nchi nzima.

“Ofisi hizi 63 zinasaidia kufanya ukaguzi na udhibiti katika masuala ya nyuklia na kuwa na vifaa madhubuti vyenye thamani ya sh. billion 2.9 na kuwa na trela la kubebea mionzi linalosaidia wafanyakazi na wananchi kuwa salama,” amesema.

Amefafanua kuwa katika ofisi hizo kuna watumishi wenye mafunzo ya kuendesha mitambo na kutoa hudumu kwa kiwango kizuri katika maeneo yote na kuifanya nchi kuwa salama wakati wote.
Amesisitiza kuwa Watanzania wanatakiwa kuwa na imani Tume yao kwa maana inafanya kazi vizuri na vifaa ambavyo wanavyo vinawapa taarifa kila siku kuhusu masuala ya mionzi na kama kuna sehemu popote nchini kuna mwanya wa kuleta athari, mapema wanapata taarifa na kudhibiti.

Amesema katika utekelezaji wa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya 2003, Serikali imefanikiwa kusajili wataalam wa mionzi wenye sifa za kutoa huduma ya mionzi kwa wananchi hakuna tatizo katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa katika miaka mitatu imesajili wataalamu 1,289 katika eneo la kutoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa, kutengeneza, kukarabati na kuendesha vifaa vya nyuklia na hilo lilikuwa halifanyiki kwa kipindi cha miaka ya nyuma.

Aidha amesema katika udhibiti matumizi salama ya mionzi, Serikali imeongeza idadi ya wanaopewa lesseni kwa asilimia 102 kutoka leseni 297 kwa 2016/2017 hadi wastani wa 767 kwa mwaka.

Profesa Busagala amesema kuwa, Serikali ya awamu ya sita imeondoa tozo na kupunguza tozo kwa kuamua kubeba gharama za upimaji (subsidy), hasa kwa wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kupunguza kutoka asilimia 0.2 ya malipwani kuwa asilimia 0.1 ya malipwani, sawa na punguzo la asilimia 50.

Pia ameongeza kuwa mafanikio mengine ambayo wamepata ni kuwa na bajeti ya milioni 400 inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kufanya tafiti na hadi zimefanyika tafiti 20 sanjari na utoaji elimu kwa wananchi.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kupeleka nje watumishi kuongeza elimu katika ya teknolojia na sayansi ya nyuklia kwa ngazi ya shahada za uzamili na kila mwaka watumishi watano wanapata fursa hiyo.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Prof. Busagala alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeongeza tengeo la bajeti ya utafiti kwa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) hadi kufikia Sh. milioni 450 katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Alisema juhudi hizo za serikali tume imeweza kupata fursa zaidi za sayansi na teknolojia ya nyukilia na pia kuwalinda wananchi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi ambapo katika miaka hii mitatu jumla ya machapisho 25 yakitafiti yamechapishwa. 

Aidha Prof Busagala aliongeza kuwa kutokana na TAEC kuwa imara kiutendaji, makusanyo yake ya maduhuli ya serikali yamepanda kutoka Sh. bilioni 8.7 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia Sh. Bilioni 10.9 mwaka wa fedha 2022/2023, ambapo mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kufungua ofisi za kanda, mipakani na kutumia mifumo ya TEHAMA kama vTANCIS, TeSWS na EDMS katika kutoa huduma.