Breaking News

TCRA WAITAKA CLOUDS TV KUWAOMBA RADHI WATAZAMAJI


Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) imetoa onyo pamoja na kuutaka uongozi wa Clouds TV kuomba radhi Watanzania kupitia taarifa zake za habari ndani ya siku tano mfululizo kuanzia leo,

Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam,  makamu Mwenyekiti wa kamati Bw Joseph Mapunda amesema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya wajumbe wa kamati kutafakari kwa kina baada ya kupitia maelezo ya utetezi yaliyotolewa na uongozi wa Clouds TV.


Amesema baada ya kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na clouds tv kuhusu kipindi chake cha Take One kilichorushwa hewani tarehe 28 June 2016 ambacho kilikiuka kanuni na sheria ya maadili ya utangazaji (maudhui) ya mwaka 2005, namba 5(b), 5(c), 5(d) na 15(c) 16(2).


“Kutokana na kipindi hicho kuwakwaza pamoja na kuwasababishia usumbufu wananchi hususan watazamaji kwa kuwasilisha mada inayozungumzia masuala ya mapenzi ya jinsia moja (ushoga), Clouds TV inatakiwa kuwaomba radhi watanzania wote na watazamaji.”
 

Amesema taarifa ya kuomba radhi itoke siku tano mfululizo katika taarifa zao za habari ya saa moja na nusu na ya saa tano usiku kuanzia siku ya kusomwa hukumu, na kwamba uthibitisho wa taarifa hizo upelekwe TCRA siku ya Jumatano tarehe 13 Julai 2016 kabla ya saa kumi jioni.
Aidha kamati hiyo pia imeutaka Clouds Tv kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha inazingatia na kufata kanuni zote za utangazaji nchini katika kutekeleza majukumu yake ya utangazaji

Akizungumza mara baada ya kutolewa tamko hilo mkurugenzi wa Clouds Media Group Bw Ruge Mutahaba amesema baada ya kutafakari kwa kina tamko la adhabu hiyo atatoa msimamo wake kama wataka rufaa au la.



“Tunaweza tukarudi nyuma na kusema tufanye kazi ya kukata rufaa, kwa sababu tunaamini na mimi nina simamia msimamo wangu kwamba tunapoambiwa tunalinda maadili ya kitaifa, kupinga jambo lolote baya ni kulinda maadili ya kitaifa,” amesema



Ameongeza kuwa “Sasa ukiambiwa kwamba ulipinga kwa namna ulivyo pinga ni tofauti kidogo labda inaweza ikasaida kutengeneza mjadala mkubwa wa kujiuliza maadili tunayotakiwa kuyalinda ni yapi.”



Mutahaba amesema “Lakini moja kati ya kitu tunachokiona kina utofauti ni kuna baadhi ya mambo yamezungumzwa ambayo sikumbuki kabisa kama yako kwenye kipindi, kwa hiyo sijui wamezitolea wapi.”



Pia amebainisha kuwa ushoga ni tatizo na kwamba lazima alikemee na ataendelea kulikemea.



No comments