MFUMUKO WA BEI WA TAIFA UMEONGEZEKA HADI ASILIMIA 5.5
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu Bw, Ephraim Kwesigabo akisisitiza jambo kwa waandishi wa
habari awapo pichani
|
....................................................................................................................................
Mfumuko wa bei wa taifa wa
mwezi Juni, 2016 umeongezeka hadi asilimia 5.5 kutoka asilimia 5.2 mwezi
uliopita kutokana na kuongezeka kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na
huduma.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephaim Kwesigabo amesema kuongezeka kwa mfumuko wa
bei kumesababishwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula
zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi.
“Mfumuko wa bei umesababishwa
na kuongezeka kwa bei za vyakula kama vile mahindi ambayo yameongezeka kwa
asilimia 3.2, unga wa muhogo kwa asilimia 2.4, samaki wabichi kwa asilimia 3.8,
maziwa mgando kwa asilimia 4.3, maharage mabichi yaliyomenywa kwa asilimia 6.1,
kitunguu swaumu kwa asilimia 12.5, njegere kwa asilimia 6.2, viazi mviringo kwa
asilimia 2.5, mihogo mibichi kwa asilimia 6.7, magimbi kwa asilimia 4.5, na
ndizi za kupika kwa asilimia 2.7,” amesema Kwesigabo.
Amesema bidhaa zisizo za
vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na huduma ya
kinywa na meno ambayo imeongezeka kwa asilimia 13.8, mafuta ya dizeli kwa
asilimia 2.4 na mafuta ya petroli kwa asilimia 4.3.
Kwesigabo amesema mfumuko wa
bei wa mwezi Juni, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia
0.5 ongezeko sawa na mwezi uliopita.
Aidha amesema mfumuko wa bei
kwa kipimo cha mwaka wa bidhaa za vyakula majumbani na migahawani umeongezeka
hadi asilimia 8.3 mwezi Juni, 2016 kutoka asilimia 7.2 mwezi Mei, 2016.
Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.47 mwezi Juni, 2016 kutoka 103.00 mwezi
uliopita.
Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa
na huduma umefikia Shilingi 96 na senti 65 mwezi Juni, 2016 kutoka mwezi
Disemba, 2015.
No comments