FEDHA ZA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU KUTOLEWA BAADA YA UHAKIKI WA WANAFUNZI HEWA
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa fedha kwa ajili ya
mafunzo kwa vitendo zitatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la
uhakiki wa wanafunzi waliombewa fedha hizo toka vyuo mbalimbali hapa
nchini.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Prof. Ndalichako aliyasema hayo
leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es
Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya ucheleweshwaji wa fedha hizo
kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Kuna zaidi ya wanafunzi 2,736
hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwemo majina ya
wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo,” alifafanua Prof.
Ndalichako.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kuna
chuo ambacho kilituma ripoti ya wanafunzi waliofukuzwa chuo mwaka
2013/2014 lakini majina hayo yametumwa tena kwa ajili ya kupewa fedha za
mafunzo kwa vitendo kwa mwaka huu.
Kutokana na kasoro zilizojitokeza
katika majina ya wanafunzi wanaotakiwa kupewa fedha kwa ajili ya
mafunzo kwa vitendo Prof. Ndalichako amesema kuwa Serikali haitatoa
fedha mpaka uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo utakapo
kamilika kwa vyuo vyote nchini.
Aidha, Mhe. Ndalichako amesema
kuwa majina ya wanafunzi hao hewa yamewekwa katika mitandao wakitakiwa
kujihakiki TCU ili kujiridhisha kama kweli ni wanafunzi na wanaendelea
na masomo.
Vile vile, Prof. Ndalichako
amevitaka vyuo vikuu kutoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa katika vyuo
vyao kufanya uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata fedha hizo kwani
kuna baadhi ya vyuo vimekuwa havitoi ushirikiano kwa kisingizio cha
kuwepo kwenye mitihani.
Aliongeza kwa kusema kuwa, vyuo
kutotoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa kufanya uhakiki wa wanafunzi
hao kutazidi kuchelewesha fedha hizo kutoka mapema.