Breaking News

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YAWEKA KIPAUMBELE SEKTA YA UTALII.

3Mwashungi Tahir- Maelezo-(Zanzibar)

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kuweka kupaumbele mbele sekta ya utalii  kwa kuwashirikisha wananchi katika mpango wa  kutekeleza  sera ya utalii kwa wote.
Hayo ameyasema  Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Dr. Ahmada Hamadi Khatib leo huko katika ukumbi wa sanaa wa  Studio ya Sanaa Rahaleo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya watembezaji Utalii nchini.
 
Amesema Utalii unahitaji kushirikiana sekta ya Habari , Utamaduni  na  Michezo ili kuweza kupata mashirikiano katika taasisi zote katika kukuza utalii nchini na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Aidha amewataka watembezaji watalii hao kuzingatia maelekezo wanayofundishwa katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuimarisha na kudumisha amani na usalama wakati wanapokuwa katika kazi yao ya kutembeza watalii.

Pia amesema ili uwe muongozajii bora ni lazima ujue unachokiongoza , kwani watalii wanatarajia kuongozwa na kufahamishwa sehemu mbali mbali za kihistoria na kutegemea kupata maelekezo kwa ufasaha zaidi.

“Watalii wanapokuja Zanzibar kutoka sehemu mbalimbali wanajua wanakuja hapa kwanza watu wake wakarimu ,tabia zetu nzuri na pia hulka zetu nzuri hivyo wajitahidi wawe watembezaji wazuri waepuke kuwafanyia udanganyifu ambao utawasababishia kuondosha uaminifu na kuondosha sifa ya Zanzibar”, amesema mwenyekiti huyo.

Sambamba na hayo amesema muongozaji mtalii anatakiwa kuwa na taaluma nzuri ambayo ataweza  kufanya wajibu wake na kufuatilia sehemu muhimu ambazo  wanazopenda kutembelea watalii.

Amewasisitizawatembezaji hao kufuata matakwa  watalii wanapohitaji  kupelekwa sehemu na  sio kufanya wanavyotaka wao kwani kuwafanyia hivyo sio ustarabu na kwenda kinyume na maadili ya kazi zao.