KAULI YA KIONGOZI WA ACT WAZALENDO ZITTO KABWE KUFATIA HOTUBA YA MHE RAIS LEO.
Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli
za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa
Vyama vingi Nchini
Tumepokea kwa MSHTUKO na
masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa
isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni. Kimsingi kauli ya Rais ni kauli
yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa
vyama vingi na kuhimiza vya vya siasa kufanya shughuli za siasa katika msimu
wote ili kuthibitisha uhai wao.
Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya
demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama chetu kitaitisha vikao vya
dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna ya kukabiliana na mashambulizi
yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.
Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoamini
katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na kujadili namna ya
kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya kulinda demokrasia nchini
mwetu.
Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za
kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa
kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi
za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini
mwetu.
Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na
Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu
kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na
kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.
Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.
No comments