Breaking News

TASAC YAENDESHA MAFUNZO KWA WADAU WA USAFIRISHAJI MAJINI MKOANI KIGOMA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali wa usafirishaji majini, tarehe Aprili 9,2025 katika ukumbi wa Kigoma Social Hall Mkoani Kigoma, kwa lengo la kuwapatia elimu ya namna nzuri ya kuendesha shughuli zao kwenye ubora wa hali ya juu. 

Akizungumza kwenye kikao hicho Afisa Mkuu Udhibiti na Usafirishaji Majini TASAC, Bw. Sylvester Kanyika amewataka wadau kutumia vyombo vya usafiri ndani ya Ziwa Tanganyika kwa kutumia weledi kuendesha kazi zao.

Bw. Kanyika ametumia fursa hiyo kuwaelekeza wadau hao kufuata maelekezo ya leseni zao ili kupunguza athari zinazotokana na kutofuata kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli zao.
“Napenda nitoe wito kwenu kufuata masharti ya leseni zenu ili muweze kufanya shughuli za kiuchumi katika ziwa Tanganyika kwa utaratibu, na kufuata maelekezo mnayopewa na wataalamu wetu kutoka TASAC,” amesema Bw. Kanyika. 

Aidha, Afisa Usafirishaji Mwandamizi, TASAC Bi. Selina Mokiti amewashukuru wadau kwa kujitokeza kushiriki mafunzo hayo na kuwaasa wadau hao kutumia weledi na maelekezo wanaoypewa ndani ya leseni zao.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Kigoma, Bw. Abdulrahman Kaponta ameipongeza TASAC kwa kuendesha mafunzo hayo kwani yamewakumbusha wadau hao hali itakayochochea kuepusha ajali na kuhakikisha wanafuata kanuni zilizowekwa.
Nao Baadhi ya wadau wa usafirishaji na mawakala wa forodha waliohudhuria katika mafunzo hayo wameishukuru TASAC kwa mafunzo hayo kwani yamekuja wakati muafaka kwa kuwa elimu iliyotolewa itawasaidia katika kuendesha shughuli zao za kila siku.

Wadau hao wameiomba TASAC kuendelea kuwapa elimu ili kuboresha kazi zao za kila siku ndani ya Ziwa Tanganyika.