Breaking News

WAZIRI KABUDI ATOA MAAGIZO SABA KWA BODI YA ITHIBATI

Na Janet Jovin - Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imetakiwa kuhakikisha kuwa, waandishi wa habari wote nchini wanazingatia sheria, kanuni, viwango vya juu vya weledi, maadili, uwajibikaji, na miongozo inayosimamia taaluma ya uandishi wa habari.

Maelekezo hayo ni kati ya maagizo saba yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi katika hotuba yake ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika tqrehe 03 Machi, 2025, katika Ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

Profesa Kabudi amesema, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari itasaidia kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hiyo, hivyo inatakiwa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali kuhusu taaluma yao.

Profesa Kabudi ameitaka pia Bodi hiyo kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo ya mafunzo ya mara kwa mara, na kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wamaadili kwa haki na uwazi.
Agizo la pili kwa Bodi ni kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, huku akisisitiza kuwa mfumo huo unatakiwa kua shirikishi na wenye kuendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.

Ameitaka JAB kuhakikisha inashirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.

Profesa Kabudi ameiagiza Bodi kuandaa programu za uelimishaji ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma ya uandishi kusimamiwa ipasavyo.

Amesisitiza kuwa ni muhimu Bodi pia ikasaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili, katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, ikiwemo kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa Habari.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi Bodi inapaswa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima, kwani Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.

Akitangaza kuzinduliwa rasmi kwa Bodi hiyo, Profesa Kabudi amesema, Serikali inatambua umuhimu wake, katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na kuahidi kuwa itaendelea kushirikiana nayo ili kuhakikisha taaluma ya habari inaimarika kwa manufaa ya taifa.

Aidha Profesa Kabudi amesema, kubobea katika eneo mahsusi kwa mwandishi wa habari, huongeza ubora wa habari na kuifanya iwe na manufaa kwa jamii, na mwandishi wa aina hiyo hujenga uaminifu kwa muda na kuwa vyanzo tegemeo vya habari.

Amesema, watazamaji na wasomaji huwategemea waandishi wa habari wabobevu kwa taarifa sahihi na za kina, kwani uwezo wao wa kutoa uchambuzi wa kina huwafanya kuwa viongozi wa mawazo katika taaluma zao na hivyo kuimarisha uadilifu wa vyombo vya habari wanavyofanyia kazi.

Profesa Kabudi amesema, waandishi wa habari waliobobea, wanapokuwa na uelewa mzuri wa mada wanazoziripoti, huwasilisha habari kwa namna inayovutia, yenye muktadha sahihi na maelezo ya kina, hivyo huifanya hadhira kuelewa vizuri zaidi masuala yanayoripotiwa, na kwa namna hiyo huboresha usomaji na uelewa wa umma.
Zaidi ya hayo, Profesa Kabudi amesisitiza kuwa vyombo vya habari na taasisi mbalimbali kuwatambua na kuwathamini waandishi wabobevu, kufungua milango ya fursa kama vile ushauri wa kitaalamu, kuhojiwa kama wataalamu, na kushiriki mijadala ya kitaaluma, hivyo kuwapa waandishi wa habari nafasi nzuri ya kukuza taaluma zao na kuwa na mchango mkubwa katika jamii.

Amesema, waandishi wa habari waliobobea, wanaweza kutumia blogu, podcast, na majukwaa ya kimtandao ili kujitambulisha kama viongozi wa mawazo katika nyanja zao, kwani kuongezeka kwa vyombo vya habari vya kidigitali kumeongeza mahitaji ya maudhui ya kitaalamu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Bodi ya Ithibati chini ya Wizara hiyo, itakuwa na jukumu la kusimamia maadili ya taaluma na kusaidia kukuza mazingira bora ya utendaji kazi katika Sekta ya Habari hapa nchini.

Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekazia kuwa Bodi hiyo itawajibika kuhimiza waandishi wa habari kuandika kwa weledi, na kuzingatia ukweli, haki na maslahi ya umma.

Amebainisha kuwa Bodi ya Ithibati yenye wajumbe saba akiwemo Mwenyekiti wake Tido Mhando, itashirikiana na Taasisis za mafunzo na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari kuhakikisha waandishi wa habari wanapata elimu bora na mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaaluma.

Akitoa shukurani zake Mhando amemhakikishia Waziri Kabudi kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wamepokea maelekezo aliyowapa na kwamba watayatekeleza kwa moyo wa uzalendo, uadilifu na ufanisi wa hali ya juu kwa ushirikiano na wadau wa sekta ya Habari.

Amesema kwa kuonyesha utayari wa kufanya kazi, vikao vya Bodi ya ithibati vitaanza Jumanne Machi 4;2025, kwa lengo la kupanga mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula, amewataka waandishi wa Habari kuilinda taaluma ya uandishi wa Habari kwa kuwa hakuna atakayeilinda zaidi ya wao wenyewe.

No comments