WASIRA - VYAMA VYA UKOMBOZI KUSINI MWA AFRIKA VIENDESHWE KWA KUZINGATIA MAHITAJI
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema vyama ya ukombozi kusini mwa Afrika viendeshwe Kwa kuzingatia mahitaji ya wakati huu bila kusahahu shabaha ya kuanzishwa kwake.
Amesema kuwa vyama hivyo vilipigania uhuru kuzikomboa jamii za waafrika ambayo ndani yake ina vizazi vilivyopo na vinavyokuja.
Wasira alieeleza hayo leo alipokuwa akifungua semina kwa viongozi vijana kutoka vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika iliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Julius Kambarage Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Vyama hivyo ni FRELIMO (Msumbuji), MPLA (Angola), ANC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia), ZANU-PF (Zimbabwe) na CCM ya Tanznaia ambapo katika mapambano ya ukombozi vilishirikiana kwa karibu na Chama cha Kikomist cha China (CPC).
Alisema lengo la semina hiyo ni kuimarisha vyama hivyo ambapo anaamini mifumo ya siasa inabadilika kutoka chama kimoja kwenda vyama vingi na lazima kutafuta mbinu ambayo itavifanya vyama hivyo kujiimarisha kutoka chini, visiwe vyama vya watu wachache hatua ambayo inalenga kuhakikisha vinaendelea kuongoza nchi zao.
“Mbinu za kuongoza nchi zao ni kuhakikisha mabadiliko yoyote ya dunia hayayumbishwi lakini pamoja na kwamba ni lazima washirikiane na dunia nyingine wasifanye dunia ikawa badala ya shabaha yao, maana duniani hapa kuna mambo yake vilevile.
“Vyama hivi shabaha yake ni ya muda mrefu ambayo ni kuona dunia ina maisha bora kwa watu wake ambao wanazaliwa kila siku, hata kama kuna mabadiliko mengi yanatokea shabaha inabaki ile ile kuona watu wetu katika nchi hizi wanapata maisha mazuri na hii ndio shabaha ya msingi na haina mwisho, huwezi kusema maisha sasa yametosha,” alisema.
Akizungumzia nafasi ya vijana, alisema ndio warithi halali wa vyama hivyo, hata yeye alikuwa kijana na hiyo inamaanisha kuwa hakuna kuendelea bila kijana.
Kwa mujibu wa Wasira, urithi wa vijana ni muhimu kwa maendeleo ya vyama hivyo na kwamba kama haikufanyika hivyo vitakuwa vyama vya wazee ambao wakiondoka na vyama vinaondoka “ni lazima kurithisha vijana ili wachukue nafasi yao katika kuongoza vyama hivyo.”
“Sio kila kijana anaweza kurithi, wanatakiwa vijana wanaojua historia, wanaojua sababu ya hivi vyama kwa nini wazee wao walipigana hadi wakafa, wakijua hivyo wataendeleza shabaha iliyowaua wale.
“Tumeanza tunachukua chipukizi na UVCCM kuwapeleka Ihemi, Iringa kuwafundisha, hapa katikati tulikuwa tumeacha hiyo program lakini sasa tumejua bila mafunzo tutapata tabu kurithisha uongozi unaoeleweka, tunawafundisha itikadi ya vyama hivi na shabaha yake,” alisema.
No comments