WANAWAKE 400 WATEMBELEA HIFADHI YA NGORONGORO NA KUSHUHUDIA "BIG FIVE"
Na Philomena Mbirika - Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani, wanawake zaidi ya 400 kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi wemetembelea hifadhi ya Ngorongoro na kushuhudia vivutio mbalimbali ikiwemo wanyama wakubwa watano maarufu kama "Big Five".
Akizungumza na wanawake hao baada ya kuwapokea leo tarehe 7 machi, 2025 Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia idara huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo amesema ujio wa wanawake hao utaendelea kuhamasisha utalii wa ndani kwenye vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
"Tukiwa tunaelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) tunatumia fursa hii kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi, na Leo kwa kushirikiana na Kampuni ya Utalii ya Tanzanite Cooperates tumepokea wanawake takriban 400 waliokuja kutalii". Alisema Mariam
Aidha, Mariam alisisitiza kuwa NCAA imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa ziara hiyo ya kitalii itatumika kuleta chachu kwa watanzania wengine ikiwa ni jitihada za Kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya kitalii ya Tanzanite Cooperates, Bi. Elina Mwangomo alisema kwamba Kampuni yake imejikita zaidi kwenye utalii wa ndani na imekuwa ikifanya ziara za kutembelea Hifadhi mbalimbali nchini ambapo bonde la kreta limekuwa sehemu pekee ambapo watalii wanaweza kujionea wanyama wengi kwa karibu zaidi ndani ya muda mfupi.
" Kreta ya Ngorongoro ni sehemu pekee ambako watalii wetu wengi wamekuwa wakivutiwa kuja kutembelea na kwa muda sasa tumekuwa tukija na makundi mbalimbali na Leo tuko na kundi la takriban wanawake 400 ambao tumekuja kutalii na kufurahi pamoja tukielekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani" Alisema Elina
Kwa upande wake Bi.Gloria Mziray kutoka Mfuko wa taifa wa bima ya Afya (NHIF) Arusha ambaye ni mmoja kati ya wanawake waliokuwa kwenye ziara hiyo alieleza kuwa safari yao ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ya kipekee sana na wamefurahishwa kuona wanyama mbalimbali waliopamba hifadhi hiyo wakiwa kwenye Mazingira yao ya Asili.
Bi. Fatuma Abduli kutoka benki ya CRDB ambao wamekuwa wadau wakubwa wa utalii nchini pamoja na kufurahishwa na upekee wa Kreta ametoa wito kwa watanzania kujenga hulka ya kutembea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya nchi.
Wakiwa katika hifadhi hiyo wanawake hao pamoja na watalii wengine waliotembelea maeneo ka Kreta ya Ngorongoro na tambarare za Ndutu wameshuhudia vivutio mbalimbali ikiwemo wanyama wakubwa maarufu kama "Big Five" ambao ni Faru, Tembo, chui, Nyati na Simba
Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yatafanyika Machi 08, 2025 Mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
No comments