WIZARA YA MADINI, UBALOZI WA CHINA WAFANYA MAJADILIANO YA UTAFITI WA MADINI
Dar es Salaam - Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian katika kikao kilicholenga kujadili fursa na maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Madini ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo kati ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango na kiongozi huyo .
Katika mazungumzo yao, Dkt. Mpango aliiomba Serikali ya China kupitia balozi huyo kusaidia shughuli za utafiti wa madini Tanzania, ambapo baada ya mazungumzo yao, Serikali ya China imetuma wataalam wawili kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti ya nchini humo ili kufuatilia na kujua mahitaji ya utafiti na maeneo mengine ya mashirikiano kati ya Tanzania na China
‘’Kikao nilichokiongoza leo Machi 3, 2025, kimejadili maeneo ya ushirikiano, na sisi kwa upande wetu tumeweza kubaini maeneo matatu muhimu ambayo Serikali ya china inaweza kutusaidia katika shughuli za utafiti na kujenga uwezo wa watumishi wa Wizara kulingana na mahitaji,’’ amesema Dkt. Kiruswa.
Maeneo matatu ambayo wataalam wa Wizara wakiongozwa na Dkt. Kiruswa waliyoweza kuyabaini ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia (high resolution airborne geophysical survey) hususani kwa kuanzia eneo la Mkoa wa Dodoma;
Maeneo mengine ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa fursa kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa ndani katika maeneo ya teknolojia za kisasa kama vile ukusanyaji na uchakataji wa taarifa za jiosayansi; na kusaidia kuleta teknolojia za kisasa za utafiti na uchakataji wa taarifa za utafiti wa madini ikiwa ni pamoja na matumizi ya ndege nyuki katika utafiti wa madini nchini.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga Kamishna, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jilojia na Utafiti wa Madini Tanzania, (GST) Dkt. Mussa Budeba, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia (GST) Dkt. Ronald Massawe, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Makamba, Makamba na maafisa kutoka ubalozi wa China nchini Bw. Chu Kun na wataalm kutoka Taasisi ya Jiolojia China Bw. Ren Junping na Bw. Sun Kai.
No comments