MHE. DKT. KHALID: SHIRIKA LA POSTA HONGERENI KWA UBUNIFU WA KIDIJITALI
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Dkt Khalid Salum Mohamed amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa kuwa wabunifu katika biashara na huduma zenye kugusa mahitaji ya sasa ya wananchi kwa kutumia kiteknolojia.
Ameyasema hayo leo tarehe 28 Februari, 2025 wakati wa uzinduzi wa Dawati la uwekezaji uliyofanyika katika ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar es Salaam, uliofanywa na Shirika kwa kushirikiana na kampuni ya Vertex International Securities na kuasa kuwa huduma hiyo iwe rahisi na wazi kwa watumiaji ili washiriki katika uchumi utakaowezesha miradi mikubwa ya maendeleo kupitia uwekezaji.
Aidha, amelitaka Shirika kutoa mafunzo kwa wananchi ili kuwajengea utamaduni wa uwekezaji miongoni mwao, pia kuongeza ushiriki wa watanzania katika Masoko ya Hisa na Mitaji na hivyo kuongeza mtaji wa ndani kwa ajili ya maendeleo
Naye kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa Dar es Salaam, Bw. Leonard Kameta ameeleza kuwa kupitia Dawati hili, usambazaji wa taarifa utaboreshwa pamoja na kuongeza uwazi katika mchakato wa uwekezaji, na kuwezesha kila mtazania kupata taarifa sahihi kwa wakati ambapo hii itakuwa na matokeo chanya, ikiongeza imani na ushirikiano kati ya taasisi za kifedha na wawekezaji kiujumla.
Kwa upande wa Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais wake Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha katika safari ya Mageuzi ya Posta yanayoendelea hivi sasa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vertex International Securities Bw. Mateja Mgeta, amelishukuru Shirika la Posta Tanzania kwa utayari wa kukumbatia dira ya uwekezaji kupitia matawi yake yote nchini, huku akisistiza kuendelea kupanua wigo wa Dawati la Uwekezaji kwa kuanzisha vituo vingi vya mawasiliano kwenye ofisi za Posta.
No comments