Breaking News

KILIMO CHATAJWA KUCHANGIA ONGEZEKO LA HEWA UKAA

Na Mwandishi wetu - Imeelezwa matumizi ya viutilifu vyenye kemikali, mbolea za viwandani na uongezaji maeneo ya kilimo unachangia asilimia 35 ya ongezeko la hewa ukaa na uharibifu wa mazingira duniani.

Aidha, uwepo wa Jarida la kilimo hai la Mkulima Mbunifu umetajwa kuongeza wakulima wanaolima kilimo ikolojia nchini.

Hayo yameelezwa na Meneja Programu ya Mawasiliano wa Biovision Africa Trust (BvAT), Fredrick Ochieng wakati akizungumza kwenye warsha ya siku moja ya wadau wa kilimo, iliyoandaliwa na Mradi wa Mkulima Mbunifu mkoani Dodoma.

Mradi wa Mkulima Mbunifu unatoa jarida la Mkulima Mbunifu kila baada ya miezi miwili, unasimamiwa kwa ushirikiano na BVAT na Shirika la Kuendeleza Kilimo Tanzania (SAT).

Ochieng amesema kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kutokana na dunia kujikita katika kilimo kisichofuata misingi ya kilimo ikolojia madhara yanayotokana na sekta hiyo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.
Meneja huyo amesema asilimia 35 ya kilimo inayochangia ongezeko la hewa ukaa na uharibifu wa mazingira inachangiwa na nchi zilizoendelea ambapo kuna wakulima wakubwa

Amesema ongezeko la hewa ukaa na uharibifu wa mazingira umesababisha nchi za Jangwa la Sahara kutumia takriban dola za Marekani bilioni 68 kwa mwaka.

“Kwa ujumla, uharibifu wa udongo unachangia kupungua kwa Pato la Taifa la Kilimo kwa asilimia 3 kila mwaka. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), kila mwaka, zaidi ya hekta milioni 10 zinaharibika,”.

Ochieng amesema athari za hali ya hewa zinazidi kuwa mbaya kati ya mwaka 2008 na 2018, ambapo mabadiliko ya tabianchi yaligharimu sekta za kilimo katika nchi zinazoendelea zaidi ya dola za Marekani bilioni 108 kwa mujibu wa (FAO 2021).

Meneja huyo amesema pia ongezeko la hewa ukaa na mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Amesema magonjwa yasiyoambukiza yalihusika na asilimia 39 ya vifo nchini Kenya mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 27 mwaka 2014.

“Baadhi ya sababu za hatari ni pamoja na ulaji wa vyakula visivyo na afya, matumizi ya tumbaku, na ukosefu wa mazoezi kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO 2019).

Pia amesema hali hiyo imechangia upotevu wa bioanuwai unaodhoofisha moja kwa moja uwezo wa kilimo kuhimili mabadiliko ya tabianchi (FAO 2019).

“Matumizi ya pembejeo na viuatilifu visivyo salama kati ya bidhaa 310 za viuatilifu zinazotumika nchini Kenya, bidhaa 195 asilimia 63 zina viambato hai moja au viwili ambavyo vimeorodheshwa kama viuatilifu hatari (HHPs), ambavyo ni asilimia 76 ya jumla ya kiasi cha viuatilifu vinavyotumika,” amesema.

Amesema madhara ya hewa ukaa na mabadiliko ya tabianchi katika Bara la Afrika yanaathiri zaidi wanawake ambapo takwimu zinaonesha ni asilimia 60 ya nguvu kazi.

Ochieng amesema mfumo wa uzalishaji wa mstari mmoja umeonyesha kuwa si endelevu na mapinduzi ya kijani yalionekana kufanikiwa mwanzoni, lakini yalisababisha mzunguko wa matatizo.

Meneja huyo amesema mifumo ya chakula ina vipengele tofauti vinavyohitaji mbinu jumuishi na hatua mbalimbali na kwamba mfumo wowote unaoharibu mazingira unazidisha hali mbaya ya upatikanaji wa chakula.

Meneja Mradi wa Mkulima Mbunifu, Erica Rugabandana, amesema elimu ya kilimo na ufugaji inayotolewa kwenye jarida hilo imeweza kuwakomboa wakulima wengi kwa kipindi cha miaka miwili.

Rugabandana amesema hadi sasa Jarida la Mkulima Mbunifu linasomwa moja kwa moja na wakulima 79,863 waliopo katika vikundi 878 nchini Tanzania.

“Jarida la Mkulima Mbunifu linatolewa kila bada ya miezi miwili ambapo hadi sasa tumeweza kufikia wakulima 79,863 moja kwa moja waliopo kwenye vikundi 878, watu 3,179 wanapokea jarida hili kwa njia barua pepe, 10,798 wanasoma kupitia Mtandao wa Facebook,” amesema.
Meneja huyo amesema hadi sasa wamechapisha kopi 144,155, habari 273 zimewekwa kwenye website ambapo wasomaji 59,263 wanasoma habari za kilimo.

Rugabandana amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima viongozi 53 ambapo 20 kati yao wameonesha mafanikio na kuwa wakufunzi wa wakulima wengine 1,082 katika Wilaya ya Meru, Karatu, Singida, Ikungi, Mbulu, Moshi DC na Hai.

Meneja huyo amesema wanakutana na changamoto ya wakulima wengi kuhitaji jarida, kukosa majibu ya sekta hiyo kupitia kwa mamlaka husika na kuchelewa kufika kwa jarida, hivyo kuwaomba wadau wengine kuunga mkono juhudi za usambazaji wa jarida la Mkulima Mbunifu.

“Lakini pia tumejifunza kuwa wakulima wengi wanaopata jarida wanasambaza elimu kwa wenzao, maofisa ugani ambao wapo kwenye maeneo ambayo jarida linafika wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima na hamasa ya kilimo ikolojia imeongezeka,” amesema

Awali akifungua warsha hiyo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sekta ya Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hoffu Mwakaje, ameshauri wadau wa kilimo ikolojia kutoa elimu na kuwa mabalozi ili kila mtu aweze kutambua faida ya kilimo hicho.

Mwakaje amesema kilimo ikolojia kinakumbana na changamoto ya soko ambapo kwa hali ilivyo ni vigumu mtu kutambua tofauti ya bidhaa zilizolimwa kwa mfumo wa ikolojia na kisicho ikilojia.

“Nimefarijika sana kwa mwamko ambao wakulima baadhi wameelewa faida za kilimo ikolojia, hivyo nawaomba kila mmoja awe ni balozi wa kilimo hiki ambacho kina faida kwa viumbe, mazingira na kiuchumi,” amesema.

No comments