Breaking News

KAMATI YA BUNGE PIC: JENGO JIPYA WMA LITAONGEZA MORALI KUWAHUDUMIA WANANCHI

🟠 Mwenyekiti Vuma ampongeza Rais, Serikali, Wizara na WMA

🟠 Katibu Mkuu asema maono ya Rais Samia utoaji huduma bora kwa wananchi yatafikiwa

Dodoma - Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma amesema kukamilika kwa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), kutaongeza morali ya watumishi katika utendaji kazi hivyo kuboresha zaidi huduma zake kwa wananchi.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, Machi 13, 2025 baada ya Kamati hiyo kuzuru na kujionea Jengo hilo jipya la kisasa lililojengwa na kampuni ya wakandarasi wazawa ijulikanayo kama Ms. Mohammedi Builders Ltd kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 6.1

“Ujio wa Mradi huu unaamsha ari ya kufanya kazi kwa watumishi na ubunifu zaidi, jambo ambalo tunaamini litaongeza tija kwa maana ya makusanyo ya Wakala, lakini pia miradi itaenda kuwasaidia Watanzania kulindwa vizuri dhidi ya watu wasio waaminifu ambao huwapunja wananchi kwenye vipimo mbalimbali,” amesema Mhe. Vuma.
Aidha, Mhe. Vuma ametoa pongezi kwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo hilo.

Vilevile ametoa pongezi kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Menejimenti yote ya Wizara pamoja na Uongozi wa WMA kwa usimamizi mzuri uliowezesha kufanikisha ujenzi husika.

Katika hatua nyingine, Mhe. Vuma amempongeza Mkandarasi wa jengo hilo na kutoa rai kwa Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mbalimbali ili fedha wanazolipwa ziendelee kubaki nchini na kuchangia katika kukuza uchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Samia kuwezesha ujenzi huo, pia amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawezesha kutimiza maono yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Hashil ameiahidi Kamati ya Bunge kutimiza maelekezo waliyoyatoa, hususan yanayohusu Wizara na WMA kuutumia muda wa mwaka mmoja wa matazamio ya jengo kwa kuhakikisha dosari ndogo ndogo zitakazojitokeza zinarekebishwa.

Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika kwa jengo, Katibu Mkuu amebainisha kuwa tayari makabidhiano yalikwishafanyika na kwamba utaratibu wa kuhamisha watumishi umekwishaanza.

Ujenzi wa Jengo hilo ulianza kutekelezwa Julai 2022 ambapo imeelezwa kuwa kukamilika kwake kutaokoa matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kinalipwa kama kodi ya pango kutokana na Wakala kutumia majengo ya kukodi kwa ajili ya Ofisi yake kuu kwa muda mrefu.

Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo umesimamiwa na Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

No comments