Breaking News

ACT WAZALENDO: BODI YA LIGI IJITAFAKARI KUAHIRISHWA KWA MECHI YA YANGA NA SIMBA

Uamuzi wa kamati ya uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kuahirisha mchezo namba 184 kati ya Young Africans (Yanga SC) na Simba SC uliokuwa uchezwe tarehe 08 Machi 2025, haukuzingatia hasara mbalimbali zilizotokana na kuahirishwa kwa mchezo huo, ikiwemo nafasi ya mashabiki, wafanyabiashara, warusha matangazo, wapenzi wa soka, na maendeleo ya soka nchini kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ibara ya 55 (2) inatoa jukumu kwa Bodi ya Ligi kusimamia ligi kuu na kuhakikisha timu zinaheshimu sheria, kanuni na maamuzi ya TFF. Kanuni namba 15 (3) inasisitiza kuwa ratiba ya ligi itatangazwa na Bodi ya Ligi na itabadilishwa tu kwa dharura au sababu za msingi. Hata hivyo, Bodi ya Ligi imekuwa ikibadili ratiba mara kwa mara bila dharura wala sababu za msingi, jambo linalosababisha hasara kubwa kwa wadau.

Kuahirishwa kwa mchezo kulitokana na madai ya timu ya Simba SC iliyozuiwa kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja kama kanuni na taratibu za mchezo wa Soka zinavyoeleza, aidha upande wa Yanga SC katika taarifa yake rasmi kwa umma ilieleza inatambua mechi ipo palepale na kwamba haitakuwa tayari kucheza mechi hiyo siku nyingine.

ACT Wazalendo inaona mwenendo huu wa Bodi ya Ligi umejaa malalamiko kutoka kwa wadau wengi, kwa kuwa imekuwa ikiongozwa na utashi wa timu hizo za Kariakoo, jambo linaloharibu taswira ya ligi yetu, heshima ya Tanzania kisoka, na kuleta hasara kwa wadhamini, mashabiki na wafanyabiashara.
ACT Wazalendo inaitaka Bodi ya Ligi iliyopo madarakani kujitafakari kama inafaa kuendelea kusimamia ligi kuu ya Tanzania au inapaswa kujiengua.

Pili, ACT WazalendoTunaitaka Bodi ya Lingi kuendesha ligi kwa kuzingatia na kusimamia sheria na kanuni bila uonevu wala upendeleo kwa timu yoyote.

Tatu, Bodi ya Ligi ichukue hatua za haraka na za haki kwa mujibu wa kanuni ya 31 (1.1 hadi 1.8), ikiwa ni pamoja na adhabu kama vile kupoteza ushindi, kushushwa madaraja mawili, kutozwa faini ya Milioni 3, na kutopata gawio la mchezo husika.

Nne, TFF ifanye tathmini ya madhara yote yaliyotokana na kuhairishwa kwa mechi hii na waathirika wote walipwe fidia.

Mwisho, ACT Wazalendo inataka kuona Mpira wa Tanzania unaendelea kukua, kupata heshima na kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmojammoja, vilabu na Taifa kwa ujumla, hatutafumbia macho matukio yote yatakayohatarisha shabaha hiyo.

No comments